Serikali kumega ekari 3000 kutoka kwenye shamba la karamagi kilosa

Na Farida Saidy- Morogoro.

Serikali
ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi
imeagiza mmiliki wa shamba la Farm Africa maarufu kama shamba la
Karamagi lililopo katika Halmashauri ya Wilaya Kilosa Mkoani Morogoro
kutoa ekari 3000 kutoka kwenye shamba hilo ili zimilikishwe kwa wananchi
wenye uhitaji wa ardhi kwa shughuli za kiuchumi.

Agizo
hilo la Serikali limetolewa Novemba 8 mwaka huu na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi alipotembelea shamba
hilo lenye ukubwa wa ekari elfu 13 ambapo hakuridhishwa na kasi ya
uendelezaji wa eneo hilo tangu Mmiliki wa shamba hilo alipomilikishwa.

“Kwa
taarifa zilizopo bwana Karamagi alimilikishwa shamba hili tangu mwaka
2012, hivyo alipaswa kila mwaka kuliendeleza shamba lake japo kwa
kiwango cha moja ya nane (1/8), hii ina maana hadi kufikia mwaka huu
ambapo umiliki wake umetimiza miaka minane alipaswa kukamilisha
uendelezaji wa eneo hili” alisema Waziri Lukuvi,

“Kutokana
na hali hii nikuagize Mkuu wa Wilaya umfikishie taarifa bwana Karamagi
kwamba mimi kama Waziri wa Ardhi namuagiza atoe ekari 3000 kutoka kwenye
shamba hili ili zimilikishwe kwa wananchi ili waziendeleze kwa shughuli
za kilimo”, alisisitiza Waziri Lukuvi.

Sambamba
na agizo hilo, Waziri Lukuvi alibainisha kuwa 2012, ni ekari 2000 pekee
ndizo zilizoendelezwa kwa kupanda mazao kati ya ekari 13,000 za licha
ya kipindi cha miaka minane kupita tangu mmiliki huyo alipopata uhalali
wa eneo hilo mnamo mwaka shamba hilo wakati alitakiwa awe ameendeleza
shamba lote kwa kipindi hicho.

Awali,
kabla ya kutoa uamuzi wa kumega sehemu ya shamba hilo ekari 3000, Mhe.
Lukuvi alisikiliza kero za wananchi wanaoishi jirani na shamba hilo
ambao wengi walimuomba kuwasaidia kupata maeneo kwa ajili ya shughuli
mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo wakitaja shamba hilo kuwa ni
sababu kubwa ya kuwakosesha maeneo ya kulima
Akiongea
na viongozi wa Wilaya ya Kilosa katika ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri hiyo, Mhe.Lukuvi alibainisha kwamba Serikali tayari
imejiridhisha kuwepo uhalali wa kufutwa mashamba 48 yaliyopo katika
Halmashauri hiyo ambayo hayajaendelezwa ili yagawiwe kwa wananchi wa
Wilaya hiyo kwa ajili ya kuyaendeleza.

Aidha,
amewataka viongozi wa Halmshauri hiyo kufuatilia mashamba mengine 24
ambayo yameonekana kutoendelezwa ili waandike ilani kwa ajili ya kuomba
kufutwa na kugawiwa wananchi wenye uhitaji.

Katika
hatua nyingine Waziri Lukuvi amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam
Mgoyi kuhakikisha suala la udalali na ukodishaji wa ardhi unaofanywa na
baadhi ya viongozi wa Wilaya hiyo na kuwakosesha wananchi maeneo ya
kilimo unakoma mara moja kwani suala hilo linapelekea kuibuka kwa
migogoro ya ardhi Wilayani humo.

Sambamba
na hayo Waziri Lukuvi amewaagiza wataalamu wa ardhi kuepuka kubadilisha
hati za umiliki wa ardhi kwa wananchi watakaogawiwa maeneo yanayotokana
na mashamba yaliyofutwa huku akiwataka wananchi kutouza maeneo
watakayopewa kwani hiyo ni huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli.
Akiendelea
kutoa maagizo mbalimbali, Waziri Lukuvi amewataka wafugaji wote
waliomilikishwa ardhi kihalali Wilayani Kilosa kuweka uzio katika maeneo
yao ili kuzuia mifugo isitoke katika maeneo yao na kuingia katika
maeneo ya wakulima ili kuepuka migogoro ya Mara kwa mara.

Amesema
wakati umefika sasa kwa wafugaji kuacha ufugaji wa kizamani badala yake
watumie maeneo hayo kufuga mifugo yao kisasa ndani ya eneo lenye uzio
ili mifugo yao iwe na tija zaidi kwao ukilinganisha na ilivyo sasa.
Waziri
Lukuvi yupo Mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ikiwa na
lengo la kupata maoni na mapendekezo juu ya kazi ya awali iliyofanywa na
tume ya uhakiki wa mashamba yasiyoendelezwa huku akishangazwa na
upendeleo ulioonyeshwa katika kuyabakiza mashamba 24 ambayo yameonekana
bado hayajaendelezwa.