Dkt. ndugulile: ukatili wa kijinsia ni ujambazi mpya

Na Mwandishi Wetu Dodoma

Naibu
Waziri wa Afya Maeandeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine
Ndugulile amesema Mwaka 2017 Tanzania ilikuwa na matukio ya vitendo vya
ukatili wa kijinsia takribani 41elfu na kati ya vitendo hivyo ukatili
dhidi ya watoto pekee ni 13 elfu.

Naibu
Waziri Ndugulile amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari
wakati wa Semina ya wabunge wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
kuhusu Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Vitendo vya Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto Jijini Dodoma.

Aidha
Naibu Waziri Ndugulile ameifananisha changamoto ya vitendo vya ukatili
Nchini kuwa ni ujambazi mpya unaozidi kuwakumba wanawake na watoto
kutokana na vitendo hivyo kuendelea kutokea katika maeneo mbalimbali
hapa Nchini.

Dkt.
Ndugulile amesema unapoongelea ukatili wa kijinsia unazungumzia maeneo
makubwa matatu ambayo ni ukatili wa kimwili, kisaikolojia na ukatili wa
kiakili na kuongeza kuwa changamoto ya ukatili wa kijinsia imekuwa
ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Ameyataja
matendo hayo yanayozidi kuongezeka kuwa ni mimba na ndoa za utotoni,
ubakaji na ulawiti dhidi ya wanawake na watoto ndio maana ili
kukabiliana na vitendo hivyo serikali tangu mwaka 2016 ilianzisha Mpango
wa Taifa wa Kutokomeza Vitendo vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

Dkt.
Ndugulile ameongeza kuwa juhudi za Serikali katika utoaji elimu bure
hapa nchini umepunguza suala la mimba na ndoa za utotoni kwa kuwa mtoto
wa kike anapozidi kukaa shuleni ndivyo uwezekano wa mimba za mapema
unapozidi kuwa mdogo.

Wakati
huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo
ya Jamii Mhe. Peter Serukamba amewambia wajumbe wa Kamati hiyo na Wizara
kuwa jamii bado ina mila potofu zinazoendeleza vitendo vya ukatili kama
vile ukeketeji na kuwataka Wabunge kuelimisha Jamii dhidi ya Vitendo
hivyo.

Aidha
Mhe. Serukamba amelitaja suala la elimu kwa umma kuhusu utokomezaji wa
vitendo vya ukatili kupewa kipaumbelae huku akisifu mpango wa Serikali
wa kutokomeza umasikini kwa kiwango cha kaya kupitia TASAF na kuongeza
kuwa umasikini pia ni chanzo cha ukatili dhidi ya wawanawake na watoto.

Naye
Mshauri Mbobezi wa Sera na Mipango kutoka Shirika la Wanawake la Umoja
wa Mataifa Tanzania Bi. Usu Malya amesema shirika lake litaendelea
kushirikiana na Wizara ya Afya Idara Kuu Maeandeleo ya Jamii kutokomeza
vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto hapa nchini.

Mpango
wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto ulianza
tangu mwaka 2016 na umewezesha kuwa na mtazamo wa pamoja katika
utekelezaji wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuondoa
mwingiliano, upotevu wa rasilimali watu, fedha na muda unaotumika
katika kushgulikia suala moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *