Serikali kutumia hekima kuwasaidia ambao wameshindwa kusajili laini zao za simu

Serikali 
imesema itatumia hekima kuwasaidia wananchi walioshindwa kusajili laini
za simu kwa sababu ya kukosa kitambulisho cha Taifa na namba licha ya
kuanza mchakato wa kupata kitambulisho hicho.


Imesema
wananchi hao ambao taarifa zao zipo katika Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA), huenda wamekosa kitambulisho au namba kwa sababu zilizo
nje ya uwezo wao.

Hayo
yameelezwa Jumapili Januari 19, 2020 na naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye katika mkutano wa ndani wa
CCM mkoani Kigoma.

“Serikali
itaona jinsi ya kutumia hekima kwa wananchi ambao taarifa zao zipo
katika ofisi za Nida kuona namna ya kufanya lakini kwa wengine ambao
hawajajaza fomu laini zao zitazimwa,” amesema Nditiye.

Amesema ambao laini zao zitazimwa ni wale waliosajili laini chache na kuacha nyingine licha ya kuwa na kitambulisho hicho.

Amebainisha kuwa usajili wa laini za simu ni endelevu licha ya baadhi ya wananchi kupuuza.