Kilichoendelea mahakamani leo kesi ya tundu lissu

Mdhamini
wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Robert Katula
ameiambia mahakama kuwa wakati anamdhamini mshtakiwa huyo hakujua kama
atapigwa risasi.


Katula
ametoa madai hayo leo Jumatatu Januari 20, katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo
ilipokuwa ikitajwa.

Amesema
Desemba 19 mwaka jana, mahakama iliamuru Lissu afike leo mahakamani
lakini amefanya juhudi za kuwasiliana naye akawafahamisha kwamba
atawasiliana na wakili wa chama lakini hadi leo kimya.

Mdhamini huyo ameomba apewe muda zaidi wa kuhakikisha anamfikisha mshtakiwa huyo mahakamani.

“Mheshimiwa
wakati natoa ahadi kwamba nitahakikisha anafika mahakamani sikujua kama
atapigwa risasi, tumemuandikia Mwenyekiti Freeman Mbowe barua atusaidie
kumfikisha mshtakiwa nchini,” amedai Katula.

Hakimu
Simba ameahirisha kesi hadi Februari 20 mwaka huu na kuamuru kwamba
mshtakiwa ni lazima afike mahakamani tarehe hiyo kabla mahakama haijatoa
amri nyingine zenye nguvu zaidi dhidi ya wadhamini.

Mdhamini wa mwingine wa Lissu ni Ibrahim Ahmed.

Kesi
hiyo ilifunguliwa Juni 14 mwaka 2016 baada ya muda mshtakiwa wa nne,
Lissu akapata matatizo yaliyomfanya ashindwe kufika mahakamani.

Mbali
na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa
gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya
Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu
na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo la kuandika habari
za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.