Serikali yasema haitaingilia kupanga bei msimu ujao wa pamba

Naibu
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuelekea msimu ujao wa pamba
serikali itajitahidi kupunguza gharama na kwamba haitaingilia kupanga
bei bali watatafuta njia nyingine za kumlinda mkulima na kuhakikisha
hapati hasara.


Ametoa
kauli hiyo bungeni leo Jumatano Novemba 6, alipokuwa akijibu swali la
nyongeza la Mbunge wa Busega (CCM), Dk. Raphael Chegeni aliyetaka kupata
tamko la serikali kuhusu wakulima wa pamba ambao waliuza pamba tangu
Mei mwaka huu lakini hawajalipwa fedha zao.

“Wakulima
wa pamba ambao mwaka hadi mwaka wamekuwa wakifanya kazi ya kulima
wamekuwa wakipata hasara kwa mfano leo hii wakulima wa Mkoa wa Simiyu
hasa wa Wilaya ya Busega wameuza pamba tangu mwezi Mei mpaka leo
hawajaliwa fedha zao sasa hauoni kwamba hii ni kuwakatisha tamaa
wakulima wasiweze kufanya kilimo kizuri zaidi na nini tamkola serikali
juu ya hili,” amehoji.

“Ninakiri
kuwa baadhi ya wakulima wa pamba hawajalipwa fedha zao, kwa mwaka huu
mpaka sasa hivi jumla ya bilioni 417 zimeshalipwa kwa wakulima wa nchi
nzima, ambao hawajalipwa wanadai bilioni 50 kufikia sasa hivi na sababu
ya msingi ni lazima tufahamu kwamba asilimia zaidi ya 80 ya pamba
inakwenda nje ya nchi, wanunuzi wetu wanakabiliwa na mtikisiko wa bei
ambao umewakabili katika soko la dunia na sisi kama nchi tulitoa
maelekezo ya bei ya kununulia na haya yalikuwa maamuzi ya serikali
kwaajili ya kumlinda mkulima asipate hasara.

“Pamba
yote iliyokuwa kwa wakulima imeshakusanywa sasa hivi kilichobaki
mikononi mwa wakulima ni tani 5,000 tu ambayo tunaamini msimu unapoanza
pamba yote ya wakulima itakuwa imeondoka, tunajitahidi kupunguza gharama
msimu huu unaokuja na hatutaingilia kupanga bei, jukumu letu litakuwa
ni kuhakikisha mkulima hapati hasara kwa kutafuta njia nyingine za
kumlinda kuliko kumuathiri mnunuzi,” amesema Bashe.