Smaujata shinyanga wafanya kongamano la kupinga ukatili jamii yahimizwa kutoa taarifa “piga simu 116”


Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mwenyekiti wa kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi
wa jamii Tanzania SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Nabila Kisendi ameiomba jamii kukemea
vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya videndo hivyo ili hatua
za kisheria zichukuliwe.

Ametoa ombo hilo katika kongamano la kupinga ukatili
ambalo limefanyika katika uwanja wa zima moto Nguzonane na kwamba limeratibiwa
na kampeni hiyo na kuhudhuriwa na viogozi wa serikali, dini, chama na wadau
mbalimbali Mkoa wa Shinyanga.

Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Nabila
Kisendi jina maarufu Madam Kisendi amesisitiza wananchi wote wakiwemo watoto na
wanawake kuungana kwa pamoja kupinga vitendo vya ukatili vinavyoendelea katika
Mkoa wa Shinyanga ili kuendeleza amani Nchini.

Aidha Mwenyekiti Madam Kisendi ametaja malengo ya
SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kuwa ni pamoja na kuhakikisha wanatoa elimu ya
kupinga ukatili kwenye jamii, Kuwatambua na kuwapongeza mashujaa wa maendeleo
na ustawi wa jamii, Kufikisha jumbe mbalimbali za Wizara na serikali kwa ujumla
kwenye jamii kupitia njia za utoaji elimu, ushirikishwaji wa wananchi kupitia
makongamano kama hili na Kujenga moyo wa uzalendo kwa watanzania, kujitoa
katika mambo ambayo yanahitaji umoja wa kijamii ili kuleta matokeo ya haraka
katika jamii zetu.

Madam Kisendi ametaja baadhi ya changamoto
zinazokwamisha kufikia malengo ikiwemo ukosefu wa ofisi kwa ajili ya kutunza
taarifa mbalimbali,ukosefu wa usafiri kwa ajili ya kufika sehemu kutoa elimu
pamoja na Ushirikiano mdogo kwa viongozi ngazi za chini.

Amesema licha ya jitihada
zinazo fanywa na serikali,taasisi binafsi na wadau mbalimbali wanatakiwa kutoa
ushirikiano ili kufanikisha kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii kwa
kutoa taarifa za viashiria vya matukio hayo.

 

Ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza afisa ustawi wa
jamii Mkoa wa Shinyanga Bi. Lydia Kwesigabo pamoja na Afisa maendeleo ya jamii Mkoa
wa Shinyanga Bwana Tedson Ngwale kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa
majukumu.

Akizungumza mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga, mtendaji talafa ya Shinyanga mjini Bwana Mathias Masalu amesema
atahakikisha changamoto zinazoikwamisha SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga anazifikisha
sehemu husika kwa ajili ya utekelezaji wake ikiwemo ukosefu wa ofisi pamoja na
usafiri ili kuifikia jamii kwa uharaka.

Amesema kuwa SMAUJATA
pamoja na wadau wengine wanatakiwa kuendelea kujituma kutekeleza majukumu yao
licha ya changamoto hizo zinazowakabili.

Wakati huo huo Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya
Shinyanga Bi. Sophia Kang’ombe  pamoja na
baadhi ya wadau waliohudhuria kongamano hilo wameisihi jamii kuacha vitendo vya
ukatili.

Kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga imefanya
kongamano la kupinga ukatili ambalo limeambatana na maandamano na kwamba limehudhuriwa
na viongozi pamoja na wadau wakiwemo wanachuo na wanafunzi wa shule mbalimbali
ikiwemo shule ya msingi Town, Mwenge pamoja na shule ya sekondari Ndala
Manispaa ya Shinyanga.