Sstaili ya tra ya kutoa elimu ya mlipa kodi “duka kwa duka” yamkosha dc wa rufiji juma njwayo

Afisa wa TRA akimuelimisha mfanyabiashara huhu (kulia) katika


stendi ya mabasi Ikwiriri, Wilayani Rufiji Mkoani Pwani leo Novemba 13,
2019 kuhusu elimu ya kodi katika maduka yao mtindo unaotumiwa na TRA
kutoa elimu ya kodi unajulikana kama “Duka kwa Duka”


Na Mwandishi wetu, Rufiji

Mkuu
wa Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani Juma Njwayo amepongeza juhudi
zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za kutoa elimu ya Kodi
kwa kuwafuata wafanyabiashara katika maeneo yao “duka kwa duka”.


Mkuu
huyo wa Wilaya amebainisha kuwa aina hii ya utoaji elimu ya kodi kwa
kuwafuata wafanyabiashara utaongeza ari ya ulipaji kodi miongoni mwa
wafanyabiasha na walipakodi wengine siyo tu katika Wilaya ya Rufiji bali
hata kwa watanzania wote.


“Niwapongeze
sana TRA kwa kuamua kufanya wiki ya elimu na huduma kwa walipakodi
katika Wilaya yetu, naamini wana Rufiji tutafaidika na elimu hii na
mapato yataongezeka”, amesema DC Njwayo.


Aidha,
Mkuu wa Wilaya amewataka wafanyabiasha na wananchi wa Wilaya ya Rufiji
kutumia fursa hii kufahamu mambo yanayohusu ulipaji kodi ili walipe kodi
kwa hiari na kwa wakati na kuiwezesha serikali kutekeleza miradi
mikubwa yenye tija kwa Taifa.


“Sote
tunashuhudia jinsi Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli anavyotekeleza
miradi mikubwa kama huu wa kufua  umeme wa Nyerere Hydro power tena upo
wilayani kwetu, kwa hiyo tutumie fursa ya elimu ya kodi na kila mmoja
aone ana wajibu wa  kulipa Kodi kwa hiari ili tupate maendeleo zaidi”,
amesisitiza Mkuu wa Wilaya Njwayo.


 DC
Njwayo  ameongeza kuwa Kodi zinazokusanywa na TRA ndizo  zinazoleta
maendeleo  ukiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kitaifa kwa
kutumia Kodi mradi wa umeme ambao utainua wilaya kiuchumi na kijamii
pamoja na kuinua hali za wananchi.


Ameongeza
kuwa ni vyema wananchi kushirikiana na TRA katika kuhakikisha kuwa
elimu watakayoipata wanaifanyia kazi na kuchangia maendeleo ya taifa
letu.


Naye
Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Honesta Ndunguru ameushukuru
uongozi wa Wilaya ya Rufiji kwa ushirikiano waliouonesha na kuwa TRA
itahakikisha inafika katika sehemu zote muhimu zenye wafanyabiasha na
kuwasajili kuwa walipakodi na kuwapatia cheti Cha utambulisho wa
Mlipakodi (TIN).


“Tutatoa
TIN kwa kila anayestahili kupata kwa ajili kufanya biashara au kupata
huduma zingine kama vile leseni ya udereva”, amesema Ndunguru.


TRA
inafanya wiki ya huduma, elimu na usajili wa walipakodi  katika mikoa
ya Morogoro na Pwani kuanzia tarehe 11 hadi 16 ili kuongeza uelewa wa
masuala ya ulipaji kodi miongoni mwa wananchi.
 Mkuu
wa Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani, Mhe. Juma Njwayo (mwenye fulana
nyeupe) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
waliofika ofisini kwake kutoa taarifa ya wiki ya huduma, elimu na
usajili wa walipakodi inayoendelea katika wilaya hiyo iliyopo Mkoa wa 
Pwani

Mkuu
wa Wilaya ya Rufiji Mhe. Juma Njwayo (kushoto) akiagana na Watumishi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania waliofika ofisini kwake kutoa taarifa ya
wiki ya huduma, elimu na usajili wa walipakodi inayoendelea katika
wilaya hiyo.