Stamico kuanzisha mradi wa kusafisha dhahabu mwanza

Imeelezwa
kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lipo katika hatua za awali
za uanzishwaji wa Mradi wa Kusafisha Dhahabu (Gold Refinery) na tayari
kampuni ya ubia ijulikanayo kama Mwanza Precious Metals Refinery Company
Limited imeanzishwa.


Hayo 
yamebainishwa  Januari 21, 2020 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa (STAMICO)
Dkt. Venance  Mwase wakati  akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini Taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji
wa Fedha za Maendeleo ya shirika hilo kwa  Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa
Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa niaba ya Waziri wa Madini.
Dkt.
Venance ameileza kamati hiyo kuwa,  mradi huo utaendeshwa kwa ubia
ambapo STAMICO itakuwa  na hisa asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75,
huku ikilelezwa kwamba, mradi huo  utakaojengwa jijini Mwanza utahusisha
kujenga mtambo wenye uwezo wa kusafisha wastani wa kilo 200 hadi 500
kwa siku.
Ameongeza
kuwa, makadirio ya fedha zinazohitajika ni Dola la Marekani Milioni
58.204 ambazo zimepangwa kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kusafishia
dhahabu, gharama za awali za mradi, kununua dhahabu kutoka katika masoko
pamoja na gharama zaza uendeshaji na kuongeza‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti
tumepanga uwe mtambo wa viwango vya kimataifa,’’.
Aidha,
Dkt. Mwase amesema kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019,
tayari mradi umetekeleza majukumu kadhaa ikiwemo kupata leseni ya
kujenga na kuendesha mtambo huo, kusainiwa mkataba wa ubia pamoja na
kuanza taratibu za uanzishwaji wa kampuni ya ubia na kupata eneo la
ujenzi wa mtambo chini EPZA. 
Ameongeza
majukumu mengine yaliyotekelezwa ni pamoja na kufanyika kwa Athari kwa
Mazingira (EIA) kwenye eneo la mradi upembuzi yakinifu pamoja na
kukusanya taarifa za upatikanaji wa dhahabu katika maeneo mbalimbali
yanayokusudiwa.
Akizungumzia
shughuli nyingine zinazoendeshwa na Shirika hilo amesema linaendelea
kutoa huduma za Kibiashara za uchorongaji miamba wa biashara katika
sekta ya mafuta na gesi ambapo katika Mwaka wa Fedha 2019/20  ambapo
limefanikiwa kupata kandarasi 4 za uchorongaji kupitia zabuni
mbalimbali  zenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 .
Kuhusu
Mgodi wa Stamigold ambao ni Kampuni Tanzu ya Shirika hilo ameieleza
kamati hiyo kuwa, kuanzia Julai hadi |Desemba, 2019, mgodi huo
umezalisha na kuuza wakia 7,133.00 za madini ya dhahabu na wakia 879.19
za madini ya fedha, vyote vikiwa na thamani ya shilingi
24,172,700,255.34.
‘’
Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hicho, mgodi umelipa jumla ya
shilingi 1,712,455, 550.91 kwa ajili ya malipo ya mrabaha, ada ya
ukaguzi na kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi,’’ ameeleza Dkt. 
Venance.
Kuhusu
mradi wa makaa ya mawe katika Mradi wa Kabulo na Kiwira, amesema jumla
ya tani 4,359.10 ziliuzwa na kulipatia Shirika kiasi cha shilingi
17,558,184.76 na kuongeza kuwa, ‘’ shirika lilifanikiwa kulipa mrabaha,
ada ya ukaguzi na tozo ya Halmashauri ya jumla ya shilingi 23,645,000.62
Aidha ameongeza kuwa Mgodi umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 400.
Kwa
upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa
hoja zilizoibuliwa na kamati, amewatoa Hofu Wajumbe wa kamati hiyo
kuhusu Maendeleo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo ameeleza
pamoja na changamoto zinazolikabili, linakua na linafanya vizuri.
Waziri
Biteko ameiomba Kamati hiyo kuendelea kuilea na kuishauri STAMICO  kwa
kuwa mwelekeo wake ni mzuri na kwamba hivi sasa lina uwezo wa kuzalisha
hadi shilingi Bilioni 20 tofauti na ilivyokuwa awali na kuongeza kuwa,
Watendaji na Bodi ya Shirika hilo mara zote wanafanyia kazi ushauri
unaotolewa na Kamati pamoja na Wizara.
‘’Mheshimiwa
Mwenyekiti, itakuwa bahati mbaya sana kulifuta shirika hili. Linakua,
wanaendelea vizuri na Wana Bodi nzuri, watendaji wanasikiliza ushauri na
kuufanyia kazi na mapungufu yanafanyiwa kazi, naomba muendelee kuilea
na kuishauri STAMICO,’’amesisitiza Waziri Biteko.