Maadhimisho ya Siku ya Ushirika
Duniani (SUD) kuanzia sasa yatafanyika katika mkoa mmoja ili kuhakikisha
kuwa wakulima na wanaushirika wanapata fursa ya kutumia maadhimisho
hayo kukutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa kuongeza
tija na masoko.
Akizungumza katika Ufunguzi wa
Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yalianza leo Jumanne, Juni
29,2021 katika Viwanja vya Nanenane Mkoani Tabora hadi kufikia kilele
chake Julai 3, 2021, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema
kuanzia mwaka huu na miaka miwili itakayofuata yatafanyika mkoani Tabora
Naibu Waziri ameeleza kuwa kufanyika
kwa Maadhimisho hayo katika Mkoa mmoja kutawezesha ushirika katika mkoa
husika kuongeza fursa za Kilimo na biashara kwa kuwa Ushirika na
biashara ni masuala yanategemeana.
Akielezea Kauli mbiu ya mwaka huu ya
maadhimisho hayo isemayo “tujijenge upya kwa ubora na tija” amesisitiza
kwamba Viongozi na watendaji wa kuwa Vyama vya Ushirika wanahitaji
kuongeza uwajibikaji wenye uadilifu na unaozingatia maadili ya kazi.
Wakati huohuo amepongeza hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa
katika kudhibiti mianya ya ubadhilifu ambazo zimekuwa zikionesha kuanza
kupungua kwa vitendo vya ubadhilifu.
“Kutokana na Juhudi zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali yetu wakati tukitathmini Siku 100 tangu kuingia
madarakani Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan tunaona vitendo vya ubadhilifu
katika baadhi ya maeneo yameanza kupungua ndio maana tunaona kuna
mabadiliko kwenye Ushirika” alisema Mhe. Bashe
Naibu Waziri ameongeza kuwa Mchango wa
Sekta ya Kilimo katika Uchumi lazima uonekane na Vyama vya Ushirika
vikiwekeza katika tija vitasaidia sana kuinua maisha ya wakulima.
Aliongeza kuwa Sekta ya inatoa ajira kwa wananchi wengi takribani
asilimia 60 hadi 80 wameajiriwa kupitia Sekta ya Kilimo na kusisitiza
kuwa Kilimo kikitumika vyema kitakuwa nyenzo ya kuondokana na umasikini
nchini.
Aidha, Mhe. Bashe ameshauri Vyama vya
Ushirika vyenye maeneo yenye wakulima wanaolima mazao aina nyingi
kujishughulisha na mazao zaidi ya mmoja badala ya Chama kuwa na shughuli
za kimsimu peke yake ili kuongeza tija ya uzalishaji na uchumi wa
wakulima wao.
“Naomba Msianzishe utitiri wa Vyama
kama eneo linazalisha mazao mengi basi Vyama vya Ushirika vilivyopo
katika eneo hilo lihudumie wakulima waliopo hapo tusifikie kuanzisha
Vyama kabla hatujatumia ipasavyo vile vilivyopo,” alisisitiza Naibu
Waziri
Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya
Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson
Ndiege amesema lengo la Maadhimisho hayo ni fursa kwa Umma kujua masuala
ya Ushirika na faida zake, changamoto wanazopitia wanaushirika na
mikakati iliyopo ya kuimarisha ushirika.
Mrajis ameeleza kuwa Tume ya Maendeleo
ya Ushirika imeendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika kuhusu umuhimu wa
upatikanaji wa huduma za ugani na pembejeo kwa wanachama kwa wakati
kupitia Vyama vya Ushirika.Akiongeza kuwa uhamasishaji huu umekuwa
ukifanyika ili kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaajiri maafisa
Ugani katika Vyama vyao ili kusaidia wakulima.Hadi kufikia mwezi
Februari 2021, Vyama vikuu vya ushirika vimeajiri maafisa ugani 75 ambao
wameendelea kutoa huduma za ugani kwa wakulima katika mazao ya tumbaku,
Korosho na Kahawa.
Dkt. Ndiege amebainisha kuwa Vyama vya
Ushirika viliagiza kupitia mfumo wa ushirika mbolea tani 22,175 zenye
thamani ya Shillingi 6,018386,364 mbegu na viwatilifu tani 252 vyenye
thamani ya Shillingi 860,645,250, mbolea tani 17,237.44. Mrajis
ameongeza kuwa uhamasishaji wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi ghalani
pamoja na huduma za Ushirika Afya kwa wakulima.