Taasisi ya moyo ya jakaya kikwete(jkci) kujenga hospitali kubwa ya moyo mloganzila

Serikali
kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) ikishirikiana na
Serikali ya China wanatarajia kujenga hospitali kubwa ya moyo katika
eneo la Mloganzila ambapo hatua za awali za mchakato wa ujenzi
zimekamilika.



Akizungumza
katika Mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI, Prof.Mohammed Janabi alieleza kuwa katika miaka minne
ya Serikali ya Awamu ya Tano taasisi hiyo imepanua huduma zake na
kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa kiwango cha kimataifa.

“Katika
kipindi cha miaka minne wagonjwa waliopatiwa huduma ni 300,836 ambao
walitibiwa na kurudi nyumbani na wagonjwa 14,960 ambao walilazwa kwa
ajili ya kupata matibabu zaidi, na mahitaji yanazidi kuongezeka hata
kutoka katika nchi jiraniani”, Alisema Prof.Janabi.

Alisema
kuwa mahitaji ya ujenzi wa hospitali kubwa ya Mloganzila yanatokana na
kuwepo kwa wagonjwa wengi nje ya nchi ambao wamekuwa wakija kupata
matibabu kwa hiyo uwepo wa hospitali hiyo kutaimarisha utoaji huduma za
matibabu ya moyo hapa nchini.

Katika
kipindi cha Miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano JKCI imeweza
kufanya upasuaji mkubwa kwa kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,537 kwa
mafanikio makubwa huku vifo vikiwa ni asilimia 6 tu sawa na wagonjwa 92
kitu ambacho kinawashawishi nchi jirani kama Uganda, Rwanda, Malawi,
Burundi na Congo DRC kuleta wagonjwa wao kwenye Taasisi hiyo.

Prof.Janabi
alisema kuwa uwepo wa vifaa vya kisasa na wataalam waliobobea
kumewezesha zoezi la upasuaji kuwa salama,  ambapo upasuaji wa moyo kwa
njia ya tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa
cathlab (catheterization), wagonjwa  4,207 walipata huduma hiyo huku
vifo vikiwa ni asilimia 1.3 tu sawa na wagonjwa 42.

“Katika
kipindi cha miaka minne huduma za JKCI zimeweza kuokoa zaidi ya
shilingi bilioni 86 kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 5,744 ambao
wangeenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na uwepo wa vifaa vyenye uwezo
mkubwa, hususani kwenye masuala ya upasuaji  wa moyo kwa njia ya tundu
dogo” Alisema Prof.Janabi.

Aidha
katika kipindi hiki cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, JKCI
imeongeza ujuzi wa wataalam ambapo kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili
barani Afrika kwa kutoa matibabu ya moyo yaliyo salama na kwa wagonjwa
wengi ikitanguliwa na Afrika ya Kusini

Aliongeza
kuwa JKCI imefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo kwa mtoto mdogo mwenye
umri wa siku 7 na mzee mwenye umri wa miaka 101 ambao kwa sasa wagonjwa
hao wote wawili wanaendelea vizuri na maisha yao.

“katika
kukabiliana na changamoto ya idadi kubwa ya wagonjwa, Rais John
Magufuli mwezi Januari 2019 alitoa nafasi kwenye jengo la watoto
lililopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kliniki za
watoto tu”, Alisema Prof. Janabi.

Prof.Janabi
alisema kuwa JKCI imenunua mashine mpya mbalimbali za matibabu ya moyo
zikiwemo mashine za kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa
umeme wa moyo  unavyofanya kazi, ventilators, cardiac monitors, test
gears, mashine ya X-ray pamoja na vifaa vya chumba cha tatu cha
upasuaji.

Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni hospitali kuu maalum kwa ajili ya
matibabu ya moyo inayomilikiwa na Serikali ambayo ilianzishwa Septemba
2015,ambayo imeendelea kuitangaza vyema nchi yetu hata katika nje ya
mipaka yetu.