Tanzania yapokea msaada wa sh. bilioni 4.2 kutoka japan kwa ajiri ya kufufua shirika la tafico

Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam

Tanzania
imepokea msaada wa Yen za Japan milioni 200 sawa na Shilingi Bilioni
4.2 kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi
Tanzania (TAFICO).

Mkataba wa msaada huo umesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu na
Kaimu Balozi wa Japan, Bw. Katsutoshi Takeda, kwa niaba ya Serikali ya
Japan.
Katibu Mkuu, Bw. Doto James, alisema kuwa msaada huo utatumika kununua
Meli ya Uvuvi yenye vifaa vya kisasa, mashine ya kutengeneza barafu,
ghala la baridi la kuhifadhia samaki, Vifaa mbalimbali vya kuvulia
samaki na vya karakana, gari lenye mitambo maalum ya barafu na Gari kwa
ajili ya kusambazia samaki.
Alisema kuwa utekelezaji wa Mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa
katika kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya
Pili (FYDP II), ambayo pamoja na mengine unalenga kuboresha Sekta ya
Uvuvi na hatimaye kuvutia Watanzania zaidi kujihusisha katika Sekta ya
Uvuvi kama shughuli kuu ya kujipatia kipato.
“Mradi huu utaongeza uuzaji wa samaki nje ya nchi, kuongeza uhakika wa
chakula nchini, na pia utaboresha usindikaji wa samaki, kuongeza thamani
na masoko na kupunguza upotevu wa mazao ya samaki baada ya kuvua”,
alieleza Bw. James.
Alisema kuwa Kiwango cha ukuaji kwa shughuli ndogo za kiuchumi za uvuvi
kilifikia asilimia 9.2 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia
8.4 mwaka 2017 ambapo kiwango kikubwa cha ukuaji kilitokana na utunzaji
mzuri wa mazalia ya samaki yakiwemo mabwawa ya watu binafsi sambamba na
kuongezeka kwa mahitaji katika soko la ndani na nje.
Bw. James alisema kuwa,  shughuli za uvuvi zilichangia asilimia 1.7
katika Pato la Taifa mwaka 2018, ambayo inadhihirisha umuhimu wa uvuvi
katika uchumi, hivyo msaada uliotolewa utachangia jitihada za Serikali
katika kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Malengo Endelevu ya
mwaka 2030 na Agenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063.
Alisema kuwa  Serikali ya Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania kupitia
misaada na mikopo nafuu katika Sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo,
Miundombinu ya barabara, Maji, Nishati Utawala Bora na Uwajibikaji
ambapo mpaka sasa Jumla ya Sh. Trilioni 1. 3 zimetolewa na Serikali hiyo
tangu mwaka 2012.
Misaada na mikopo hiyo inadhihirisha kuwa kuna uhusiano mzuri wa
kirafiki kati ya Tanzania na Serikali ya Japan, hivyo matumaini ni kuwa
urafiki huo utaendelea kuimarishwa na Serikali zote mbili kwa ajili ya
maendeleo ya nchi hizo.
Kwa upande wake Naibu na Kaimu Balozi wa Japan, Bw. Katsutoshi Takeda,
kwa niaba ya Serikali ya Japan amesema nchi yake itaendelea kuisaidia
Tanzania kutokana na ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili lakini
pia kuchangia jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi na
kuondoa umasikini wa wananchi wake.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamahtamah
ameishukuru Serikali ya Japan kwa msaada huo utakaosaidia kufufua
Shirika hilo la Uvuvi.
Alisema kuwa Serikali itapeleka mswaada Bungeni mwezi Januari mwakani,
ili kuliwezesha TAFICO kuanza kazi zake rasmi na kwa kishindo ili
Shirika hilo liweze kuchangia katika uchumi wa Taifa kwa kiwango
kikubwa.
Alisema kuwa pamoja na msaada huo, Serikali imechukua hatua za kuchambua
mali zilizokuwa zikimilikiwa kinyemela na baadhi ya taasisi na watu
ambapo mpaka sasa mali zenye thamani ya zaidi shilingi bilioni 118
zimerejeshwa Serikalini na kazi ya kurejesha mali nyingine zinaendelea
kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina.