Mkurugenzi uzalishaji wa Kiwanda Cha AtoZ, Binesh Harria akimuonyesha Msaidizi wa Balozi wa Denmark nchini, Lena Hothes pamoja na wageni wengine hatua za Uzalishaji wa Taulo za kike kiwandani hapo |
Seif Mangwangi
Arusha
TANZANIA imeingia katika historia nyingine baada ya Kiwanda maarufu cha AtoZ chenye Makao yake Makuu Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha kuingia rasmi makubaliano ya uzalishaji wa Taulo salama za Kike na kampuni ya Kimataifa ya Real Relief ya Nchini Denmark.
Makubaliano hayo yamefanyika leo Mei27, 2024 katika kiwanda cha AtoZ Ungalimited na kushuhudiwa na Mwakilishi wa balozi wa Denmark nchini, Msaidizi wake namba moja Bi. Lena Hothes pamoja na viongozi kutoka Tamisemi , ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Katika utiaji saini makubaliano hayo, Kiwanda Cha AtoZ kimewakilishwa na Mkurugenzi wa Uzalishaji Binesh Harria huku kampuni ya Real Relief ikiwakilishwa na Mkurugenzi wake wa ufundi, Torben Holms.
Amesema Taulo hiyo yenye jina la SAFE PAD pakti yake moja inaweza kutumika kwa miaka miwili tangu iliponunuliwa kwa kuwa mtumiaji atakuwa akiifua mara baada ya kumaliza matumizi yake na kuanika na Kisha kurudia kuivaa tena.
” Hii ni bidhaa nyingine mpya ambayo tunaenda kuizalisha hapa hapa nchini kwetu, imeshapimwa na kuthibitishwa ubora wake na Mamlaka zote nchini ambazo ni TMDA na TBS na tayari tumeanza uzalishaji wake, itakuwa ni bidhaa nafuu kabisa kwa mtumiaji” anasema na kuongeza:
” Mfano kwa Mwanafunzi anayeingia kidato Cha kwanza, akinunua pakti mbili za safe Pad anaweza kuzitumia Hadi anamaliza kidato Cha nne kwa kuwa atakuwa akivua na kuifua Kisha kuitumia tena na bila kupata madhara yoyote, hii imeshapimwa na ubora wake kudhibitishwa,”anasema.
Anasema kwa kuanzia kiwanda kitakuwa kikizalisha Taulo elfu mbili (2000), kwa siku na baada ya miezi nane hadi kumi kiwanda kitaanza kuzalisha Taulo elfu kumi (10,000) kwa siku na uzalishaji utaendelea kuongezeka zaidi kulingana na uhitaji wake. “Baada ya kutosheleza soko la ndani tutanza kuuza katika Mataifa mengine kwa kuwa uhitaji ni mkubwa sana,” anasema.
Msaidizi namba Moja wa ubalozi wa Denmark nchini, Lena Hothes akikagua Taulo za kike alizozawadiwa |
Amesema mtoto wa kike kushindwa kutumia Taulo wakati wa hedhi kutokana na gharama zake kuwa kubwa ni tatizo ambalo limekuwa likikabili mataifa mengi Duniani, hivyo ujio wa Taulo ya Safe Pad ni mkombozi kwa Tanzania na Mataifa mengine.
Mwakilishi wa kampuni ya Real Relief ya Nchini Denmark, Torben Holms, akionyesha ubora wa Taulo za Kike zinazozalishwa kiwandani hapo |
Amesema Taulo hiyo ina ubora wa hali ya juu kwa kuwa inauwezo wa kufyonza hedhi kwa haraka na Haina muwasho wa aina yoyote na ni urafiki wa Mazingira tofauti na Taulo nyingi ambazo zinatumika hivi sasa.