Tbs yajipanga kutoa huduma za papo hapo katika maonesho ya sabasaba

 

Mkuu
wa kitengo cha Uhusiano na Masoko (TBS) Bi.Gladness Kaseka akizungumza
na waandishi wa habari katika ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
leo Jijini Dar es Salaam.

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
limewataka wafanyabiashara na wajasiriamali nchini kujitokeza katika
Maonesho ya biashara ya kimataifa ya 45 Sabasaba yanayotarajiwa kuanza
Juni 28 katika Viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es
Salaam.

Akizungumza leo katika Ofisi za TBS
Jijini Dar es Salaam Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Masoko (TBS)
Bi.Gladness Kaseka amesema kuwa kutakuwa na huduma ambazo watakuwa
wanatoa papo hapo kulinganisha na maonesho ya kipindi kilichopita kama
huduma ya usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi vitatolewa
papo hapo

“Tutawapa msaada wa kujisajili kwenye
mfumo ambapo ilikuwa ni changamoto ambayo wamepitia kwa muda mrefu
tutawasaidia kujisajili kwenye mfumo pia tutawapatia mkaguzi palepale na
kuweza kwenda kukagua mazingira yao ya biashara na kuwapatia kile
kibari ndani ya siku moja”. Amesema Bi.Gladness.

Aidha Bi.Gladness amesema kipindi
chote hicho cha Maonesho wafanyabiashara wanaopeleka biashara na bidhaa
nje ya nchi watapata huduma na taarifa mbalimbali za masoko ya bidhaa
zao ili kuepuka vikwazo vya biashara wanapokua wakifanya biashara nje ya
nchi.

Pamoja na hayo Bi.Gladness amewataka
wale ambao wanahitaji huduma za viwango kufika katika maonesho hayo
kwasababu kutakuwa na huduma za kuuza viwango katika banda lao pia
watatoa elimu kwa wadau mbalimbali wa viwango.