Tbs yawatembelea wajasiriamali wa wilaya ya liwale mkoani lindi na kutoa elimu ya viwango


Wakaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakikagua baadhi ya maduka ya vyakula na vipodozi pamoja na viwanda vya wajasiriamali wilayani Liwale mkoani Lindi.
TBS imeanza kampeni ya kutoa elimu kwa wajasiriamali na wenye viwanda juu ya umuhimu wa kupata alama ya ubora sambamba na kukagua na kusajili maduka ya vyakula na vipodozi kwa mkoa wa Lindi .


***************************************

Na Mwandishi Wetu, Liwale

WAJASIRIAMALI na wenye viwanda wilayani Liwale mkoani Lindi wametakiwa kujitokeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya kupata alama ya ubora, hatua ambayo itawawezesha kuondokana na vikwazo vya kibiashara na kupanua wigo wa soko la bidhaa zao.

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti jana na leo na maofisa wa TBS, wakati walipowatembelea wajasiriamali pamoja na wenye viwanda na kuzungumza nao katika maeneo yao ya biashara kwa lengo la kuwahamasisha wajitokeza TBS kupata alama ya ubora.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa leo, Afisa Usalama wa Chakula wa TBS, Barnabas Jacob, alisema wapo wilayani Liwale kwa ajili ya kazi hiyo pamoja na kufanya ukaguzi.

“Kwa hiyo tunatoa wito kwa wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kuthibitisha ubora wa bidhaa zao TBS hatua itakayowezesha bidhaa zao kuondokana na vikwazo vya kibiashara,” Jacob.

Alisema wanachotakiwa kuwa nacho ni barua ya utambulisho kutoka SIDO na baada ya hapo wakifika TBS mchakato unaanza mara moja, hivyo ni muhimu kwao kuchangamkia fursa hiyo.

Jacob alifafanua kwamba alama ya ubora kwa wajasiriamali inatolewa kwao bure na shirika hilo, kwani gharama zote zinalipwa na Serikali, hivyo wanachotakiwa wao ni kupitia SIDO kwa ajili ya kupata barua ya utambulisho.

Pia, Jacob alisema wamefanya ukaguzi wa awali kwa wenye viwanda ambavyo wazalishaji wake wanataka kupata alama ya ubora.

Alitaja miongoni mwa viwanda ambavyo maofisa hao wa TBS wamefanya ukaguzi na kuhamasisha kujitokeza kupata alama ya ubora kuwa ni pamoja na vile vinavyokamua mafuta ya alizeti, viwanda vya kubangua korosho, kwenye mashine za kusaga unga pamoja na kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za mikate.

“Wote hao tumewafikia na kuwahamasisha kuja kupata alama ya ubora TBS” alisema Jacob.

Aidha, alitaja kazi nyingine ambayo wameifanya wilayani humo kuwa ni pamoja na kukagua na kusajili maduka ya vipodozi na chakula ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kukidhi matakwa ya sheria za nchi na kulinda afya za walaji..

Alisema usajili majengo ya biashara unawapa wafanyabiashara uhakika wa kutunza bidhaa na kwamba wanasajili jengo kulingana na bidhaa zinazoenda kuhifadhiwa humo.

Usajili wa bidhaa, majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara bila vikwazo.