Tcb benki yapeleka neema kahama kwa wakulima wa tumbaku


Wakulima wa zao la Tumbaku wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kukaa mkao wa kula kunufaika na huduma ya benki ya biashara Tanzania (TCB) katika huduma za Kilimo kupitia benki hiyo.

Hayo yamesemwa Leo na Mkurugenzi wa mikopo wa benki hiyo Henry Bwogi kutoka makao makuu ya benki hiyo wakati akiongea na waandishi wa Habari wilayani Kahama.

Bwogi amesema kuwa benki ya TCB imejipanga vizuri kuwahudumia wakulima wa Tumbaku wilayani Kahama Kwa kuwasaidia wakulima kwenda kwenye Kilimo Cha Kisasa pamoja na kuviinua vyama vya Ushirika.

Ameongeza kuwa dhamira kuu ya benki ya TCB ni kutengeneza mnyororo wa thamani kati ya wakulima,Vyama vya Ushirika,wanunuzi wa mazao na masoko Ili kuleta tija na faida kubwa Kwa pande zote.

Sambamba na Hayo Bwogi amesema kuwa Benki ya TCB imejipanga kuwainua wauzaji wa pembejeo wilayani Kahama Kwa Kuwapa mikopo itakayowawezesha kusogeza pembejeo Kwa wakulima na kujenga maghala ya kuhifadhia mazao.

Kuhusu uzoefu wa huduma za benki ya TCB na Kilimo Bwogi amesema kuwa wanafanya kazi katika mikoa ya kusini Kwa zao la Korosho,Mbeya eneo la Kyela Kwa zao la Mpunga pamoja na Mkoa wa Kagera Kwa mazao ya Kahawa,Maharage na ufugaji.

Amesisitiza kuwa Wakulima watanufaika na huduma za Benki ya TCB Kwa kupata huduma za Kasi na haraka,gharama nafuu za huduma,kupata bima za majanga mbalimbali na kuwaunganisha wakulima na masoko katika mnyororo wa thamani na huduma ya bima ya Afya kupitia NHIF.

Benki ya biashara Tanzania (TCB) Ina matawi themanini na Mbili (82) nchini kote katika mikoa na baadhi ya wilaya huku ikitoa mikopo ya vikundi,mikopo binafsi,mikopo ya biashara ndogondogo na kati.

Mikopo mingine ni mikopo ya biashara pamoja na mikopo ya wastaafu ambayo Kwa Tanzania ndiyo benki ya kwanza kuuanzisha mikopo hiyo.