‘‘ubunge si saizi yangu’-rc makonda

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Na Richard
Mwaikenda
MKUU wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ‘ubunge si saizi yake’ kuliko cheo kikubwa
alicho nacho cha ukuu wa mkoa.
RC Makonda
amewananga watu ambao kila akifanya jambo la kimaendeleo ndani ya wilaya tano
za mkoa huo, wana fikra potofu kwamba anafanya hivyo kwa lengo la kutaka
kugombea ubunge 2020.
RC Makonda,
aliyasema haya hivi karibuni alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji wa
jiwe la msingi ujenzi wa jengo la kisasa la ghorofa moja la CCM Wilaya ya
Kinondoni, Dar es Salaam. Pia aliahidi kujenga majengo kama hilo katika wilaya
za Ilala, Ubungo, Temeke na Kigamboni yatakayogharimu zaidi y ash. Bil. 2.
Alisema kuwa
nafasi aliyonayo ya ukuu wa mkoa ni kubwa kuliko ubunge, kwani ana mamlaka
makubwa kuliko hata wabunge  kumi waliopo
katika mkoa anaouongoza.
Aidha,
Makonda, amesema kuwa hata katika baadhi ya vikao au mikutano ya mkoa
anayoongoza, wabunge hawawezi kuongea bila kupata ridhaa kutoka kwake.
“Kuna watu
wana fikra potofu  wakiona ofisi
inajengwa wataanza kufikiri cheo cha ubunge. Cheo nilichonacho ni kikubwa mno
kuliko ubunge, mimi nikikaa kwenye kikao changu, wabunge wote kumi wanaomba  ruhusa ya kuongea kwangu,’alisema Makonda
huku akishangiliwa na wana CCM waliofurika katika hafla hiyo.
“Maana yake
nina majimbo yote kumi Dar,
Siamini kama
kuna mwana CCM mzalendo ambaye anaweza kuhusisha kazi zangu na  ubunge wa jimbo moja.Wajibu wangu ni
kuwatumikia wananchi wote bila kusahau CCM iliyomuweka madarakani Rais Magufuli,”
alisema Makonda.
“Hizi nafasi
zipo  na zinakuja kwa ratiba za Mwenyezi
Mungu, lakini wajibu wangu ni kufanyakazi niliyopewa na Rais John Pombe
Magufuli ya kuwatumikia wananchi wote bila kusahau chama kilichotuweka
madarakani.”
“Msingekuwa
nyie wana CCM, kusimama imara kutafuta kura; kukubali kutukanwa, kuzomewa na
hata wengine kuvuliwa nguo mkipita maeneo mbalimbali ikiwemo  Kariakoo, lakini mlisimama imara kumpigania
Rais John Magufuli, sasa ni wakati wenu wa kula matunda ya jasho lenu, wala mimi
siwezi kukaa kwenye kiti na kusahau jasho mlilotoa, nakumbuka ugumu na jasho
mlilotoa mwaka 2015,” alisema Makonda.
Aliwasihi
wana CCM kuendelea kujenga umoja, mshikamano na uzalendo kwa CCM na kwamba
ofisi anazojenga  ni alama  na kielelezo cha mapenzi  na utiifu wake kwa chama chake kilichomlea.
“Sina sababu
ya kujificha, mimi si mteule ambaye anakionea haya Cha Cha Mapinduzi. Mimi ni
mteule ambaye nafurahia na kuji-proud ya kwamba ni  zao la ccm,” alisema Makonda ambaye amelelewa
na Umoja wa Vijana wa CCM.
Alisema kuwa
tangu ateuliwe katika nafasi hiyo amefanya mambo mengi ya maendeleo, huku
akitaja baadhi ya miradi kama; Ujenzi wa Jengo la upasuaji Hospitali ya
Mwananyamala, Hospitali ya Chanika, Jengo la Uzazi Hospitali ya Amana Ilala,
utengenezaji magari ya polisi, kugharamia matibabu ya watoto 200 wenye matatizo
ya moyo.