Uhamiaji yawatia mbaroni watuhumiwa 03 wanaofanya shughuli za kughushi huduma za kiuhamiaji

Idara ya Uhamiaji Tanzania inawashikilia Watuhumiwa watatu (3) wanaojihusisha na vitendo vya kughushi huduma mbalimbali za kiuhamiaji.

Akiongea na Waandishi wa Habari mapema leo hii katika Ofisi ndogo za Uhamiaji Makao Makuu Dar se salaam Msemaji Mkuu wa Uhamiaji Mrakibu Paul John Mselle alisema, Watuhumiwa hao walikamatwa jana tarehe 16 Juni 2020 majira ya saa saba usiku   katika eneo la Somanga Wilaya ya Kigamboni na Mbagala Wilaya Temeke katika Jiji la Dar es salaam

Watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na oparesheni inayoendelea hivi sasa ya kuwasaka watuhumiwa wanaojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuhamiaji.

Hii ni kutokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wageni kudai kuwa wanatapeliwa na baadhi ya watu wanaojitambulisha kama maofisa Uhamiaji na wanawapa huduma       ambazo siyo stahiki.

“Tulipowafanyia upekuzi watuhumiwa hao, tuliwakuta na vifaa mbalimbali vya kiuhamiaji” alisema

Miongoni mwa vitu vilivyokamatwa ni pamoja na Mihuri 2 ya Uhamiaji inayotumika kugonga ndani ya pasipoti wakati mtu anaingia na    kutoka nchini (Exit & Entry stamp) ya nchi ya Afrika ya Kusini

Mihuri 2 ya Uhamiaji inayotumika kugonga ndani ya pasipoti wakati mtu aningia na   kutoka nchini (Exit & Entry stamp) ya nchi ya Malawi, Mihuri 2 ya Uhamiaji inayotumika kugonga ndani ya pasipoti wakati mtu aningia na   kutoka nchini (Exit & Entry stamp) ya nchi ya Mauritius, Mihuri mbalimbali 18 ya Idara ya Uhamiaji Tanzania.

Vifaa vingine vilivyokamatwa ni Kompyuta mpakato 3, aina  Dell 2 na HP 1, Zantel Moderm 2 na Smile 4G LTE 1, Flash Disk Genx 8 @4GB, Sumsung Hard Disk  1, CPU Dell 1, Pasipoti ya Nigeria 1 yenye Namba A08894918, CD 10 na kanda 01 ya redio.

Aidha zinashikiliwa pia Simu 4 aina TECNO, Simu 2 aina ya Sumsung, Simu 1 aina ya INFINIX, Simu 1 aina ya VIFONE, VIVO 1, HONOR 1, Stamp Pad 3, Mikasi 5 na Fedha Taslimu kiasi cha Tsh2,914,960/=

Mrakibu Mselle aliendelea na kusema kwamba, Kwa sasa watuhumiwa wote watatu (3) wanashikiliwa na Idara ya Uhamiaji na kwa   kuwa makosa yao yanaangukia kwenye Uhujumu uchumi basi watakabidhiwa kwa vyombo vingine vya Dola kwa hatua zaidi za kisheria.

Hata hivyo ametoa wito kwa watanzania kushirikiana na Idara ya Uhamiaji katika kufichua    wahalifu ikiwemo wahamiaji haramu na watu ambao mwenendo wao hapa nchini siyo mzuri kwa kutoa taarifa katika ofisi za Idara ya Uhamiaji zilizo karibu nao au ofisi nyingine za serikali ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.

Aidha amewakumbusha watanzania na wageni kwamba huduma za kiuhamiaji zinapatikana katika ofisi za Uhamiaji zilizopo nchi nzima na si vinginevyo pia mtu anaweza kupata huduma hizo kupitia tovuti  ya idara ya  Uhamiaji www.immigration.go.tz