Ulega azitaka taasisi za bima na fedha kuwa mkombozi wa wafugaji na uvuvi

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Abdallah Ulega akifungua kikao cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na
uvuvi (hawapo pichani) ambapo amezisisitiza kampuni za bima na taasisi
za kifedha kuwasaidia wafugaji. Kikao hicho kimefanyika leo Juni 17,
2021 jijini Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo), Dkt. Bedan Masuruli akizungumza wakati wa kikao cha
wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi kilichofanyika leo Juni 17,
2021 jijini Dodoma .

Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi,
Bw. Stephen Michael akielezea kazi inayofanywa na dawati wakati wa kikao
cha wadau wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi kilichofanyika leo Juni
17,2021 jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau
wa bima kwa ajili ya mifugo na uvuvi wakifatilia hotuba ya Naibu Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani) kilichofanyika
leo Juni 17,2021 jijini Dodoma

Na.Alex Sonna,Dodoma

Taasisi za bima na za kifedha
zimetakiwa kuwa mkombozi kwa wafugaji na wavuvi kwa kuhakikisha wanakuwa
na uwezo wa kuwa na bima ya mifugo na samaki itakayowasaidia kuwa na
ulinzi wa uwekezaji wao na kuweza kukopesheka.

Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega leo Juni 17, 2021 wakati akifungua
kikao cha Wadau wa Dawati la Sekta Binafsi ambalo lipo chini ya Wizara
ya Mifugo na Uvuvi kikao hicho kimefanyika leo Juni 17,2021 jijini
Dodoma.

Ulega amesema kuwa wafugaji na wavuvi
wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kutokopesheka kirahisi na
taasisi za kifedha na hivyo kuwafanya washindwe kuitumia fursa ya mikopo
ambayo ipo ili kukuza mitaji yao na hatimaye kuongeza mitaji na kipato
pia.

“Kutokana na changamoto hii, wizara
imeona ni vema kuwakutanisha wadau wanaohusika ili wote kwa pamoja
tujadili tatizo nini na nini kifanyike ili tutakapotoka hapa tuwe na
suluhisho ambalo litajibu tatizo la wafugaji na wakulima kuhusu bima na
mikopo,” alisema Ulega.

Ulega amesema kuwa mifugo na samaki ni
uwekezaji na ni bishara kubwa hivyo taasisi hizi za bima na fedha
lazima ziwe na mtazamo huo na kwamba kufanya kazi na wafugaji na wavuvi
kutawaletea tija na wao wenyewe.

Lengo la wizara ni kuhakikisha
uwekezaji na biashara kwenye sekta za mifugo na uvuvi zinakua na mchango
wake katika kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla
kinaongezeka. Vilevile amezishauri taasisi za fedha kuangalia uwezekano
wa kupunguza riba kwenye mikopo ili wafugaji na wavuvi waweze
kukopesheka kirahisi.

Vilevile amesisitiza kwa wataalam na
wadau walioshiriki kikao hicho kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na
wavuvi ili watambue kuwa mifugo na samaki walionao ni uwekezaji. Pia
amesema biashara na uwekezaji ukishamiri na kukiwa na mazingira mazuri
kila mtu atataka kuwekeza na kufanya biashara ya mifugo na samaki pamoja
na mazao yake.

Naye Kaimu Katibu Mkuu
anayeshughulikia sekta ya mifugo, Dkt. Bedan Masuruli amesema kuwa sekta
za mifugo na uvuvi zinahitaji kuendelezwa na moja kitu kinachotakiwa ni
mitaji hivyo kupitia kikao hicho anaamini kuwa tatizo la upatikikanaji
mitaji litapatiwa majibu.

Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael amesema dawati
lilifuatilia upatikanaji wa bima kwa wafugaji ili kuweza kuwasaidia
wafugaji na wavuvi kupata mikopo. Shirika la Bima la Taifa (NIC),
limetoa bima kwa vyama vya ushirika vya wafugaji vitatu na vyama vya
ushirika vya wavuvi vitatu.

Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti,
na Maendeleo ya Masoko ya Bima Tanzania, Bw. Muyengi Zakaria amesema
kuwa wameshazielekeza kampuni zote za bima nchini waandae bidhaa ambazo
zinakidhi mahitaji ya wafugaji na wavuvi. Lakini pia ni lazima kuwepo na
muongozo ambao utawasaidia wafugaji na wavuvi kuhakikisha wanakata bima
itakayowasaidia wakati wanapopatwa na majanga.

Kikao hicho cha wadau kilihudhuriwa na
wawakilishi wa taasisi na kampuni za bima, taasisi za kifedha,
wawakilishi wa vyama vya ushirika vya wafugaji na wavuvi pamoja na
viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.