Wadau chunya watakiwa kushikamana kulinda watoto

Na Joachim Nyambo,Chunya.
WADAU
wilayani Chunya mkoani Mbeya wametakiwa kushikamana kwa pamoja ili
kudhibiti matukio ya ukatili dhidi ya watoto yanayoonekana kushamiri
wilayani hapa huku watekelezaji wa matukio hayo wakiwa ni watu wa karibu
wakiwemo wazazi.
Katika
siku za hivi karibuni wilaya ya Chunya imekumbwa na matukio kadhaa ya
ukatili dhidi ya watoto na wengi wa wahanga wa matukio hayo ni watot
walio na umri wa chini ya miaka mitano wanaohitaji uangalizi wa karibu
kutoka kwa jamii inayowazunguka.
Image result for ukatili watoto chunya
Ofisi
ya Ustawi wa jamii wilayani hapa imekiri kuwa vitendo vya ukatili dhidi
ya watoto vimekithiri wilayani hapa na sasa vinatishia maisha ya watoto
na kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kuwanusuru na vitendo
hivyo.
Afisa
Ustawi wa Jamii Wilaya ya Chunya, Theresia Mwendapole alibainisha hayo
alipozungumza na mwandishi wetu juu ya tukio la hivi karibuni la
mwanamke mmoja wilayani hapa kumchomo moto makalio mwanaye wa kike wa
kumzaa mwenye umri wa miaka miwili na miezi saba kutokana na kile
alichodai mtoto huyo kuwa na tabia ya kujisaidia hovyo(kujinyea).
Kwa
mujibu wa Theresia mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Agatha
Julius(21) mkazi wa kata ya Itewe wilayani hapa anashikiliwa na Jeshi la
Polisi wilayani hapa wakati mtoto akiendelea kupata matibabu hospitali
ya wilaya na atakapopona mtuhumiwa atakabidhiwa Polisi ili hatua zaidi
za kisheria ziendelee kuchukuliwa dhidi yake.
Afisa
huyo alisema tukio hilo lilitokea mwezi jana nyumbani kwa mzazi huyo
katili aliyedai kuchoshwa na tabia za mwanaye za kwenda haja hovyo.
Theresia
alisema baada ya ofisi yake kupata taarifa za tukio hilo kutoka kwa
majirani wema waliolibaini walifika nyumbani ambapo walimchukua na
kumuwahisha katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya alikolazwa kwaajili ya
matibabu.
Hata
hivyo afisa huyo anasema kinachomsikitisha ni kuwa licha ya ofisi yake
kutumia nguvu kubwa kutoa elimu kwa jamii juu ya malezi bora ya watoto
hasa wadogo bado vitendo hivyo vinashamiri wilayani hapa.
“Hivi
karibuni mwanamke mmoja alikamatwa kwa tuhuma za kumuua na kumzika
porini mwanawe eneo la Igundu.Wilaya hii kila siku ukatili dhidi ya
watoto wadogo unaongezeko”alisema Theresia.
Kwa
upande wao baadhi ya majirani wa mama aliyemchoma moto makalio mwanaye
akiwemo Kissa Kayuni walisema kitendo kilichofanywa na mama huyo si cha
kiungwana hasa ikizingatiwa huyo ni mwanawe wa kumzaa.
Naye
mjumbe wa Kamati ya usalama wa mtoto Wilaya ya Chunya Mchungaji Elisha
Mwakabana alisema wazazi wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu kwa kuhudhuria
nyumba za ibada ili watu waepukane na matendo maovu katika jamii.
Diwani
wa Kata ya Itewe,Alex Kinyamagoha aliwaonya wananchi kuacha tabia za
kujichukilia sheria mkononi kama alivyofanya mwanamke huyo kwani baadae
wahanga wanaweza kulipiza kisasi.