Wadau wa madini ya tanzanite waafiki zuio la utoaji tanzanite ghafi

 
WADAU wa madini ya
Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,
wameunga mkono uamuzi wa Serikali wa madini ghafi ya Tanzanite
kutotolewa nje ya ukuta unaozunguka migodi hiyo bila kuongezwa thamani
ifikapo Novemba mosi mwaka huu.
 
Wadau wa madini ya
Tanzanite wakiwemo, wamiliki wa migodi, wachimbaji, wanunuzi, madalali,
wachakataji, wafanyabiashara na maofisa wa Tume ya madini, walikutana
jana kwenye ofisi za madini Mirerani.
 
Mmoja kati ya
wachimbaji madini hao, Samuel Rugemalira alisema suala la kuhifadhi
madini ndani ya ukuta ili yaongezwe thamani ni zuri kwani kutakuwa na
usalama zaidi tofauti na kuyaweka nyumbani.
 
Rugemalira alisema
yeye ameelewa vizuri maelezo ya serikali yaliyotolewa kuhusu katazo la
kutoa ndani ya ukuta unaozunguka migodi, madini ghafi bila kuongezwa
thamani.
 
Ofisa habari wa
shirikisho la vyama vya wachimbaji madini nchini Femata Dk Bernard
Joseph alisema serikali inapoamua kufanya jambo lake lazima itakuwa
imejipanga kikamilifu katika utekelezaji wake.
 
Mwenyekiti wa mamlaka
ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo alisema miundombinu ya
kufanikisha zoezi hilo inapaswa kuandaliwa kwani uzalishaji ukifanyika
kwenye migodi mingi kutakuwa na changamoto.
 
Mchimbaji mwingine
Elisafi Lema alisema siyo jambo baya kutunza madini ndani ya ukuta ila
siyo madini yote yanayofaa kuongezwa thamani.
 
Ofisa madini mkazi wa
mkoa wa kimadini wa Simanjiro, Daudi Ntalima alisema uamuzi huo una
manufaa makubwa kwa wadau wa madini na serikali kwa ujumla.
 
Ntalima alisema
wachimbaji wa madini ya Tanzanite watafaidika zaidi wakifanya biashara
pindi wakiuza madini yasiyo ghafi ambayo yameongezwa thamani.
 
Aliwataka wadau wa
madini kuanza mchakato wa kujenga ofisi kwani wameshatenga maeneo ya
ndani ya ukuta huo kwa ajili ya zoezi hilo.