Wafanyabiashara wametakiwa kusajili bidhaa na majengo ya vyakula kuendana na matakwa ya sheria

 

 Afisa
udhibiti ubora wa TBS Bw. Anderson Msumanje akimsikiliza Mkurugenzi
Mkuu wa wa TPRI Dkt. Ephrahim Njau alipotembelea banda la TBS.
Afisa Uhusiano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi Neema Mtemvu
akitoa elimu kwa wadau mbalimbali waliotembelea katika banda la TBS
kwenye maonesho ya nne ya mifuko na programu za uwezeshaji wananchi
kiuchumi yanayoendelea mkoani Arusha. 

 Katika
maonesho haya wananchi wamepata fursa ya kupata elimu ya Viwango na
kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS. Mtemvu alitoa wito kwa
wajasiriamali na wafanyabiashara kwenda TBS kusajili majengo ya vyakula
na vipodozi na kuthibitisha bidhaa ili waweze kupata masoko ya uhakika .


Wananchi wakipata fursa ya kupata elimu ya Viwango na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS.




Na Mwandishi Wetu, Arusha


SHIRIKA
la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiasha kujitokeza kusajili
bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi ili kuwawezesha kufanya
shughuli zao kwa kukidhi matakwa ya sheria za nchi na kulinda afya za
walaji.


Wito
huo umetolewa na afisa uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu kwenye Maonesho ya
Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyoanza
Ferbruari 7, mwaka huu hadi 13 jijini Arusha yakiwa yameandaliwa na
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).


Shirika
hilo linashiriki maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu ya viwango kwa
wananchi, wajasiriamali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali na
msisitizo wao mkubwa ni ujenzi wa Tanzania ya viwanda na kukua kiuchumi.


“Tunatoa
wito kwa wanaofika kwenye maonesho haya kusajili bidhaa na majengo ya
vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria ambayo imetokana na mabadiliko
ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019,” alisema Mtemvu.


Sheria
hiyo ilirudisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na
vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Dawa na Chakula
Tanzania (TFDA).


“Kwa
hiyo usajili wa bidhaa, majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la
kisheria ili kuwawezesha kufanyabiashara zao urahisi,” alisema Mtemvu
wakati akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa wananchi waliotembelea
banda la shirika hilo kwenye maonesho hayo.


Alisema
usajili majengo ya biashara unawapa wafanyabiashara uhakika wa kutunza
bidhaa na kwamba wanasajili jengo kulingana na bidhaa zinazoenda
kuhifadhiwa humo.


Kwa upande wa usajili wa bidhaa, Mtemvu alisema eneo linalohusika ni bidhaa za chakula na vipodozi .


Alisema
usajili wa vipodozi unalenga kuhakikisha vipodozi vilivyopigwa marufuku
kwenye soko la Tanzania haviingizwi nchini kutokana na kuwa na viambata
sumu.


Wakati
huo huo, Mtemvu ametoa wito kwa wajasiriamali kujitokeza kwa wingi
kuthibitisha ubora wa bidhaa zao TBS bure, kwani gharama hizo zinalipwa
na Serikali kwa lengo la kuwawezesha kufanyabiashara.


Alisema
wanachotakiwa kuwa nacho ni barua ya utambulisho kutoka SIDO na baada
ya hapo wakifika TBS mchakato unaanza mara moja. Alisema wamefurahishwa
na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye maonesho hayo