Wafungisha ndoa watakiwa kujisajili kwenye e-rita

KABIDHI Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Bw Frank Kanyusi  akisisitiza jambo kwa Waandishi wa habari  juu ya umuhimu kwa wafungishaji ndoa wote hapa nchini kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali wa eRITA  ambapo mwisho wa kujisajili ni Juni 10, 2024.

Na Mwandishi Wetu

KABIDHI Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi amewataka wafungishaji ndoa wote hapa nchini kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali wa e-RITA ifikapo Juni 10, 2024.

“Mfumo huu wa kidijitali utawazeshesha kutambulika katika kanzidata ya Msajili Mkuu wa Ndo na Talaka sambamba na kupata leseni mpya za kidijitali za kufungisha ndoa,” amesema Kanyusi na kuongeza kuwa mfumo utaongeza ufanisi na kuongeza udhibiti wa usajili wa ndoa.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana,  Kanyusi alisema walengwa katika zoezi hilo ni wafungishaji wote kutoka dini na madhehebu yote nchini na kwamba usajili wa kundi hilo siyo utaratibu mpya kwani umekuwa ukifanyika kwa miaka mingi kupitia mfumo wa analojia.

“Kuanzia Januari mwaka huu mpaka sasa tayari wafungishaji ndoa 3,635 wameshajisajili kwenye mfumo wa e-RITA. Naomba nitoe rai kwa wale ambao bado kujisajili kwenye mfumo kufanya hivyo kwani shahada  za ndoa zitatolewa kwa wale tu waliosajiliwa katika mfumo,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Kabidhi Wasii Mkuu, zoezi hilo la usijili  linawahusu wafungishaji wote hata wale ambao walishasajiliwa awali kwenye mfumo wa analojia ikijumuisha walio na leseni hai na ambao leseni zao zimekwisha muda wake kutumika hivyo kuhitaji kuhuishwa.

Aidha, Kanyusi amebainisha kwamba kuanzia sasa wafungishaji ndoa wapya watatakiwa kutumia mfumo mpya  wa kidijitali wa e-RITA na kupata leseni zinazowapa mamalaka kisheria ya kufunga ndoa.

“Ili kujisajili wafungishaji ndoa wanatakiwa kuingia kwenye tovuti ya Wakala yaani www.rita.go.tz kisha bofya kitife kilichoandikwa e-RITA na kuchagua huduma ya Ndoa na Talaka baada ya hapo utapata maelekezo,” amesema.

Akifafanua zaidi, Kanyusi amesema zoezi la usajili linahusisha ujazaji wa taarifa binafsi za mfungishaji ndoa, dini na dhehebu lake na pia atahitaji kuthibitishwa  na viongozi wa dhehebu lake.

“RITA imeendelea kufanya maboresho katika utoaji wa huduma zake kwa njia ya kielekroniki kwa lengo la kuongeza ufanisi sambamba na kusogeza huduma zake karibu na wananchi pamoja kufikia matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” ameongeza.