Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo wakati
akifunga mkutano wa nne wa mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa
mwaka 2021 ulioandaliwa na Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), jijini
Mwanza.
Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza na uongozi wa
Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), katika mkutano wa nne wa
mashauriano wa wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021 ulioandaliwa na
Bodi hiyo, jijini Mwanza.
Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza na wadau
kutoka Benki ya CRDB ambao wanatoa mikopo kwa wakandarasi wazawa ili
kuweza kupata mitaji ya kutekeleza miradi mikubwa nchini, baada ya
kufunga mkutano wanne wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi jijini
Mwanza.
Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewataka wakandarasi
wazawa kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa kuomba na kutekeleza zabuni
za miradi ya Serikali inayotangazwa kwani kwa kufanya hivyo kunapelekea
kutekeleza miradi hiyo chini ya kiwango au wakati mwingine kushindwa
kabisa kuimaliza.
Aidha,
Waitara ameeleza nia ya Serikali kuendelea kuwapa miradi mingi
wakandarasi wazawa lakini lazima waoneshe uwezo wao kwa Serikali kwa
kutekeleza miradi waliyopewa tayari kwa mifano ili Serikali iendelee
kuwadhamini.
Ameyasema
hayo jijini Mwanza wakati akifunga mkutano wa nne na wa mwisho wa
mashauriano na wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa mwaka 2021, ulioandaliwa na
Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ambapo pamoja na mambo mengine
amesisitiza miradi inayotolewa kwa wakandarasi wazawa itekelezwa kwa
ubora na viwango kama ilivyo katika mikataba na thamani ya fedha
ionekane.
“Nawasihi
msitoe rushwa katika kuomba miradi, mshirikiane, muache ubinafsi ili
muweze kupata miradi mikubwa na kuitekeleza kwa pamoja, kama kuna
changamoto mikutano mikubwa kama hii ndio mahali sahihi ya kuzungumzia
utatuzi wa changamoto hizo”, amesisitiza Waitara.
Ameongeza
kuwa ni muhimu kwa wakandarasi wazawa kushiriki miradi mikubwa
inayofanywa na wakandarasi kutoka nje ili waweze kuwa wabobezi kwenye
kazi hizo na wakati mwingine miradi kama hiyo inapohitaji kufanyiwa
ukarabati inaweza kufanywa na wakandarasi wa ndani badala ya kuwaachia
wakandarasi wa kigeni kuja kuendelea kutekeleza miradi hiyo.
Kwa
upande wake Msajili wa CRB, Rhoben Nkori, amemuambia Naibu Waziri
Waitara kuwa Bodi yake itafanya majumuisho ya maazimio yote ya mikutano
minne iliyofanyika na kuyawasilisha Wizarani kwa ajili ya kupatiwa
utatuzi wa changamoto na kuona namna bora ya kuwawezesha wakandarasi hao
hasa katika miradi inayotarajiwa kutangazwa.
“Mheshimiwa
Naibu Waziri jumuiya ya wakandarasi inapenda kukushukuru kwa
kushirikiana nasi katika mikutano yetu miwili ya Arusha na hapa Mwanza,
na kwa niaba ya wenzangu napenda kukuahidi kuwa maelekezo yako yote
uliyotupatia kwenye vikao hivi viwili tunakwenda kuyafanyia kazi”,
amesema Nkori.
Jumla
ya wadau 1,366 wa Sekta ya Ujenzi wameshiriki katika mikutano minne ya
mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi katika mikoa ya Arusha, Mbeya,
Dar es Salaam na Mwanza ambapo kati ya hao wakandarasi ni 1,035 na wasio
wakandarasi 336.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi