Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Walimu (TSC), Moses Chitama (katikati), akifafanua masuala mbalimbali
kuhusu wajibu na haki za Walimu, katika mkutano wa pili wa Umoja wa
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), Dodoma,
Januari 7, 2021.
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Walimu (TSC), Moses Chitama (Meza Kuu), akifafanua masuala mbalimbali
kuhusu wajibu na haki za Walimu, katika mkutano wa pili wa Umoja wa
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, Dodoma, Januari 7, 2021.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo
ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mecktildis Kapinga,
akizungumzia kuhusu upandaji madaraja kwa walimu, wakati wa mkutano wa
pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo
pichani), uliofanyika jijini Dodoma, Januari 7, 2021.
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Walimu (TSC), Moses Chitama (kulia) akifafanua jambo kwa Mwalimu Raymond
Lyoba kutoka Urambo, Tabora, muda mfupi baada ya kuwasilisha mada
kuhusu haki na wajibu kwa walimu katika mkutano wa pili wa Umoja wa
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), Januari
7, 2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo
ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mecktildis Kapinga
(katikati), akifafanua jambo kwa Mwalimu Huruma Muya kutoka Kigamboni
Dar es Salaam (kushoto) na Mwalimu Simon Mwemutsi kutoka Ifakara
Morogoro (kulia), muda mfupi baada ya kuwasilisha mada kuhusu haki na
wajibu kwa walimu katika mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa
Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), Januari 7, 2021 jijini
Dodoma.
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Walimu (TSC), Moses Chitama (wa tatu-kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa
Ajira na Maendeleo ya Walimu wa Tume, Mecktildis Kapinga (wa
tatu-kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa
mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania
Bara, muda mfupi baada ya kuwasilisha mada kuhusu haki na wajibu kwa
walimu, Januari 7, 2021 jijini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa mkutano wa pili wa
Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, wakifuatilia
mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, Januari 7, 2021.
Na Veronica Simba
Serikali imewahamasisha Walimu wa Shule
za Msingi na Sekondari nchini, kujiendeleza kielimu katika ngazi
mbalimbali ili kuboresha zaidi utendaji wao wa kazi.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma leo,
Januari 7, 2021 na Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC),
Moses Chitama wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Umoja
wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara.
Akifafanua, amesema kuwa, kujiendeleza
kielimu ni haki ya msingi kwa watumishi wote wa umma wakiwemo walimu,
ndiyo maana Serikali kupitia Tume imekuwa ikiwahamasisha kuitumia fursa
hiyo ipasavyo.
Chitama amekemea tabia ya baadhi ya
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania
Bara, ambao hukataa kutoa ruhusa kwa watumishi walio chini yao wenye nia
ya kujiendeleza kielimu.
Hata hivyo, Kaimu Katibu huyo amesisitiza
kuwa Walimu wote wa shule za umma wenye nia ya kujiendeleza kielimu,
wanapaswa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Mamlaka ikiwemo kufuata
Mpango wa Mafunzo.
Aidha, amewasisitiza kuhakikisha wanapata
ruhusa ya maandishi kutoka kwa Wakuu wao, kabla ya kwenda masomoni
kwani kinyume chake watakabiliwa na mashtaka ya utoro kazini ambayo
adhabu yake ni kufukuzwa kazi.
“Tumekuwa tukipata rufaa nyingi za kesi
za Walimu ambao walitoroka kazini na kwenda masomoni hivyo kufukuzwa
kazi. Serikali inapenda walimu msome lakini fuateni taratibu
zilizowekwa,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa
Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Mecktildis Kapinga, akifafanua
kuhusu utaratibu wa kupanda vyeo, ameueleza Mkutano huo kuwa, kanuni
inaelekeza kutompandisha cheo mtumishi yeyote wa umma akiwa masomoni,
hadi pale anapohitimu ndipo mchakato wa kumpandisha hufanyiwa kazi.
“Naomba mtambue kuwa utaratibu huo ni kwa
watumishi wote wa umma, na siyo kwa walimu pekee kama ambavyo baadhi
yenu mmekuwa mkinung’unika,” amefafanua Kapinga.
Mkutano huo wa siku tatu, ulianza Januari
5, 2021 huku ukiongozwa na kaulimbiu isemayo uongozi na usimamizi
makini wa elimu, utaimarisha Tanzania katika uchumi wa kati.
Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya
Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za msingi na sekondari Tanzania
Bara, walio kwenye utumishi wa umma.