Wamshukuru magufuli kuwaondolea kero ya maji

Na Moha

Mwenyekiti Kijiji cha Matela, Elias Njita (kushoto)akitoa salam za shukran kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajengea mradi wa maji mbele ya Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akimsikiliza mkazi wa Kijiji cha Matela, Naombi Mbotela akieleza adha waliyokuwa nayo kabla ya kujengewa mradi wa maji.


Meneja wa RUWASA Wilaya ya Magu, Mhandisi Anna Mbawala (katikati) akiwasilisha taarifa ya mradi wa Matela kwa Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani). Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli na kulia ni Meneja RUWASA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Immaculata Raphael.

Wananchi wa Kijiji cha Matela, Wilayani Magu wakifurahia mradi wa maji wakati wa ziara ya Naibu waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani) kwenye mradi huo.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Matela Wilayani Magu wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji wilayani caption

med Saif- Magu


Wananchi wa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza wamemshukuru Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kuwaondolea kero ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya majisafi
na salama.

Shukrani hizo zimetolewa Agosti 15, 2020 wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ya kukagua mradi wa maji wa Matela katika kijiji
cha Matela wilayani humo.

Awali, Aweso alisema ziara yake imelenga kutembelea miradi ambayo
wakandarsi wake wamechelewa kuikamilisha kwa wakati kama inavyoelekeza
mikataba yao.

Alibainisha kuwa Matela ni miongoni mwa miradi uliyoisumbua Wizara ya Maji
kwani ujenzi wake ulichukua muda mrefu na hivyo kuwacheleweshea wananchi
kupata huduma ya maji kinyume na azma ya Rais Dkt. John Magufuli.

“Tangu anaingia madarakani, Rais Magufuli aliazimia kuwaondolea kero ya
maji wananchi wake, kuna baadhi ya miradi inakwamisha azma hiyo kufikiwa kwa
wakati ukiwemo huu wa Matela ambao hata hivyo nafarijika kuona sasa nao
umekamilika,” alisema Aweso.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Waziri Aweso, wananchi wa
Matela walisema licha ya kwamba mradi huo umechelewa kukamilika kwa wakati
lakini umeleta faraja katika maisha yao.

Naomi Mbotela, Mkazi wa kijiji cha Matela alimshukuru Rais Magufuli kwa
kuwapatia mradi huo ambao alisema umewaondolea kero ya kutembea umbali mrefu
na kutumia muda mwingi kufuata huduma ya maji.

“Kwa sasa hatuna shaka kwenye suala la maji, zamani sisi wanawake
tuliteseka sana, tulikua tunatoka Saa 11 alfajiri na kutembea umbali mrefu
kufuata maji na hii wakati mwingine ilitusababishia migogoro kwenye ndoa
zetu,” alisema Mbotela.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Matela, Elias Njita alisema uwepo wa mradi
huo ni uthibitisho kuwa Rais. Dkt Magufuli ni Rais wa wanyonge.

“Tunamshukuru sana Rais kutuona na kutujali sisi wanyonge huku vijijini,
ametoa fedha nyingi kutujengea huu mradi ili sisi wanyonge tupate maji,”
alisema Njita.

Aliahidi kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli hasa ikizingatiwa kwamba
kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya  vijijini wamekuwa
wakisahaulika.

“Tunaahidi sisi tutamuunga mkono Rais, tunaahidi hatutomuangusha kazi
anayofanya ni kubwa na ni ngumu sisi wanyonge tulikua tumesahaulika lakini
yeye anatujali ili na sisi tuweze kujikwamua kimaendeleo,” aliongeza
Njita.

Aidha, kwa mujibu wa msimamizi wa mradi Meneja wa Wakala ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilayani Magu, Mhandisi Anna Mbawala ni kwamba
ulianza kutekelezwa na Mkandarasi M/S STC Construction Company Ltd Mwaka
2017 na ulipaswa kukamilika 2019 na kuwa umetekelezwa kupitia Mpango wa
Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) kwa gharama ya shilingi milioni
397.9.

Alibainisha kwamba ulianza kutoa maji rasmi tarehe 02 Agosti, 2020 na kuwa
umekabidhiwa kwa Jumuiya ya watumiaji maji ya Nyanguge-Muda kwa ajili ya
kuhudumia wakazi wapatao 5,000 wa Kijiji cha Matela na vitongoji
vyake.