Wananchi kigoma kunufaika na kilimo cha umwagiliaji kupitia uendelezwaji wa bonde la luwiche

 

Picha ikionesha machimbo ya Kifusi katika eneo la Mahembe, kifusi
ambacho kitatumika katika Ujenzi wa Miundombinu ya Kilimo cha
Umwagiliaji katika Bonde la Luwiche

Picha ikionesha machimbo ya kokoto katika eneo la Simbo malighafi ambayo
itatumika katika ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji katika
bonde la Luwiche katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma

.Picha ikionesha machimbo ya mchanga katika eneo la Kagongo, mchanga
utakaotumika katika ujenzi  wa miondombinu ya kilimo cha umwagiliaji
katika Bonde la Luwiche katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.

Na Mwandishiwetu – Kigoma.

Wananchi
katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma hususan katika vijiji vya
Kamara,Simbo,Machanzo,Nyomoli na Kasuku wanategemea kunufaika na kilimo
cha umwagiliaji kupitia mradi mkubwa wa uendelezwaji wa bonde la Luwiche
unaotegemea kuanza mapema mwakani.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Miundombinu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi,Mkama Kimasa
amesema kuwa Serikali imeshafanya makubaliano na Serikali ya Kuwait juu
ya utekelezaji wa mradi huo na eneo la hekta elfu tatu ambazo zipo
kwenye mkataba zinategemea kuendelezwa katika maana ya kujenga
miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, na mchakato wa kutafuta mzabuni
umeanza.

Mhandisi Kimasa amesema,mradi huo utagharimu kiasi cha fedha za mkopo zaidi ya shilingi Bilioni ishirini mpaka kumalizika.

Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kamara moja ya kijiji
kitakachonufaika na Mradi huo, Bw. Omary Katura akizungumza kijijini
hapo amesema, wananchi wa kijiji hicho wanategemea kupata mafanikio
makubwa endapo mradi huo utatekelezeka kwa kuwa wananchi wameshaukubali
mradi huo.

 “Tunasubiria tuu Wizara na Taasisi husika waje kuanza
ujenzi haraka kwasababu na sisi wenyewe tumeshafika katika maeneo ambapo
wanategemea kufanya ujenzi na tukajiridhisha kuwa hakuna matatizo sana
ambapo changamoto ni ndogo tuu za kawaida ambazo ni njia za kupitisha
vifaa hivyo mpaka maeneo ya site.” Alisema

Kwa upande wake Afisa
Umwagiliaji wa Wilaya hiyo Bwana Sudi Hussein amesema,kwasasa wakulima
wana lima kwa kutegemea msimu wa mvua na wanaweza kulima kwa vipindi
viwili tofauti hivyo endapo mradi huo utafanikiwa wakulima wataweza
kulima mara tatu kwa mwaka na kupata faida zaidi,

Mazao yanayolimwa kwa sasa katika Bonde hilo ni Mpunga, Mahindi na mazao mengine ya mboga mboga.