WANANCHI NGORONGORO KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAKAZI.

WANANCHI NGORONGORO KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAKAZI.

Egidia Vedasto

APC Media, Arusha.

Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wametakiwa kujiandikisha Katika Daftari la Wakazi ifikapo Oktoba 11hadi Oktoba 20 kufuatia tangazo lililotolewa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jijini Arusha, Mchengerwa amesema, kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ya nchi, kifungu cha 16 na 18, sura 288 kwa tangazo la serikali 673 na 674 yalihusisha Wilaya ya Ngorongoro kufutwa na sasa yamerejeshwa kuendelea kupata huduma zote kama ilivyokuwa hapo awali ikiwemo haki ya Demokrasia.

“Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wanastahili huduma zote za kijamii na kiuchumi kama wananchi wengine wote nchini, hivyo wana haki ya kujiandikisha katika daftari la wakazi na kuwachagua viongozi sahihi muda utakapowadia” amefafanua na kuongeza,

“Nitoe wito kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro, kwa kata, vijiji na vitongoji vyote kuzingatia tangazo hili la mgawanyo wa maeneo ya kiutawala, kujiandikisha na kuchukua fomu za kugombea ili wenye sifa waweze kuchaguliwa na kutetea maendeleo ya Taifa” amesema Mchengerwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Ngorongoro Marekani Bayo ameishukuru Serikali kwa tangazo hilo linalowapa wananchi wa Ngorongoro kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Wilaya ya Ngorongoro ina vijiji 65, vitongoji 242, na sasa kazi kubwa ni kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi kufanya maamuzi yaliyo sahihi itakapofika 27 Novemba, 2024” ameeleza Bayo.

Hata hivyo Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Monduli Happiness Laizer amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Monduli kuhusu kujiandikisha katika daftari la Wakazi na kubainisha kwamba wanatumia viongozi wa mila na machapisho ili kuharakisha zoezi hilo.

“Katika wilaya yetu ya Monduli tuna kata 20, vijiji 62, na vitongoji 236 vitakavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kwa kasi hii tunavyoendelea kutoa elimu wananchi wameelewa na wako tayari kufanya maamuzi ifikapo Novemba 27 mwaka huu” amesema Laizer.