Wananchi wa kahama wamshukuru rais magufuli kwa kuwachangia ujenzi wa shule

 Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack (Mwenye ushungi wa njano),
Katibu Tawala Mkoa Bw. Albert Msovela (mwenye suti nyeusi), Kaimu Mkuu
wa Wilaya ya Kahama Mhe. Jasinta Mboneko na Viongozi wengine wakiwa
kwenye moja ya vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Mayila ambapo
wanafunzi wa darasa la kwanza wameanza masomo yao hapo tarehe 06
Januari, 2020. 
Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza na wananchi
wakiwemo wazazi na walezi (hawamo pichani) waliokuwa shuleni Mayila
kuwachukua watoto wao baada ya muda wa masomo
Shule
ya msingi Mayila iliyopo Mtaa wa Mayila, kata ya Nyihogo Wilaya ya
Kahama imefunguliwa rasmi huku wananchi wa kata hiyo wakimshukuru Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa
kuwachangia shilingi mil. 5 ili kuhakikisha shule hiyo inakamilika.
Wazazi
hao wametoa shukrani hizo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Zainab Telack alipokwenda kukagua utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais la
kuhakikisha shule hiyo inafunguliwa mapema jana tarehe 07 Januari, 2020.
Wamesema
kuwa, kukamilika kwa shule hiyo kutawapunguzia adha ya umbali wa zaidi
ya kilomita 3 watoto wa kata hiyo waliokuwa wanalazimika kuvuka barabara
kubwa kufuata shule kata za jirani hali iliyopelekea kuwa katika hatari
ya kugongwa na magari.
“Nashukuru
sana kwa shule hii, watoto wetu mwanzo walikuwa wanakwenda mbali na
sisi kama wazazi tupo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kujenga
maboma”
 amesema Bw. Richard Joseph.
Diwani wa kata ya Nyihogo Mhe. Shadrack Mguami amesema, “kuna
wakati naamka usiku kumuombea Mhe. Rais, sikutegemea kupata fedha
kutoka kwake kwani angeweza kufanya shughuli nyingine lakini akaona atoe
hapa, tunaahidi tutaendelea kumuunga mkono kwa kujenga maboma”
Naye
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama Mji Bw. Anderson Msumba amesema
watoto zaidi ya 200 wameandikishwa kuanza darasa la kwanza hivyo uhitaji
ni mkubwa, hata hivyo Halmashauri inaendelea kukamilisha maboma 108 na
kufunga shule mpya 8.
“Tunamshukuru Mhe. Rais ametupa mori kuhakikisha shule hii inafunguliwa” amesema Msumba.
Mhe.
Rais alichangia shilingi milioni 5 ili kuongeza nguvu ya kukamilisha
shule hiyo alipopita Wilayani Kahama akielekea Wilayani Chato mwezi
Novemba, mwaka jana 2019 na kuagiza ifunguliwe mwezi Januari mwaka huu
2020.
Shule hiyo iliyokuwa na vyumba viwili vya madarasa, hivi sasa ina vyumba 8 na matundu ya vyoo 12.