Wanaume wahofia wake zao kurogwa wakigombea nafasi za uongozi


Mjumbe wa Baraza la Wanawake CCM (UWT)
wilaya ya Meatu, Avelina Mwigulu akizungumza wakati wa warsha ya
ufuatiliaji wa kazi za uhamasishaji wa jamii juu ya umuhimu wa wanawake
kushiriki katika nafasi na michakato ya maamuzi na uongozi iliyoandaliwa
na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kukutanisha pamoja wadau kutoka
makundi ya viongozi wa mila,dini na jamii kutoka mikoa ya Shinyanga
(Kishapu),Kigoma (Kasulu), Tabora (Uyui), Mara (Tarime) na Simiyu
(Meatu) lengo likiwa ni kuongeza nafasi za wanawake katika nafasi za
uongozi. Alisema wanaume wenye hofu ya Mungu wanapata hofu kuwaruhusu
wake zao kujihusisha na masuala ya siasa kwamba watajihusisha na masuala
ya ushirikina. Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), wilaya ya
Meatu Elizabeth Kabati akizungumza katika warsha hiyo ambapo alisema
baadhi ya wanawake wamekuwa wakishindwa kugombea nafasi za uongozi kwa
hofu ya familia zao kurogwa.
Mjumbe wa Kitengo cha wanawake katika Chama cha Walimu wilaya ya
Meatu,Christina Paga akiwasilisha matokeo ya kazi za uhamasishaji wa
jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi na michakato ya
maamuzi na uongozi zilizofanywa na wadau mkoani Simiyu. Aliitaka jamii
kuacha kuhusisha uongozi wa mwanamke na imani za kishirikina.
Katibu Kinyaki Teachers SACCOS Meatu Rahel Silvester akizungumza katika
warsha hiyo ambapo aliwataka wanawake kujiamini na kutokata tamaa ili
kufanikiwa kushika nafasi za uongozi katika jamii.
Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa nguvu za pamoja (TAPO) TGNP Grace Kisetu
akizungumza wakati wa warsha ya ufuatiliaji wa kazi za uhamasishaji wa
jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi na michakato ya
maamuzi na uongozi.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog 
Imeelezwa kuwa baadhi ya wanaume wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wanaogopa
kuwaruhusu wake zao kugombea nafasi za uongozi ikiwemo siasa wakihofia
kuwa watajihusisha na masuala ya imani za kishirikina.
Hayo yamebainishwa na wadau wa haki za wanawake kutoka mkoa wa Simiyu
katika Warsha ya ufuatiliaji wa kazi za uhamasishaji wa jamii juu ya
umuhimu wa wanawake kushiriki katika nafasi na michakato ya maamuzi na
uongozi iliyofanyika Jumapili Februari 16,2020 katika Ukumbi wa Vijana
Center Mjini Shinyanga.
Mjumbe wa Baraza la Wanawake CCM (UWT) wilaya ya Meatu, Avelina Mwigulu
alisema wanaume wenye hofu ya Mungu wanapata hofu kuwaruhusu wake zao
kujihusisha na masuala ya siasa kwamba watajihusisha na masuala ya
ushirikina.
“Baadhi ya wanaume wana imani potofu kuwa mtu yeyote anayetaka kuwa
kiongozi lazima aende kwa mganga wa kienyeji, hivyo wanasema mama
anapoanza kuchukua fomu kugombea,lazima aende kwa waganga akagangwe
ndiyo maana wanaume wenye hofu ya Mungu wanahisi wake zao watajihusisha
na vitendo vya ushirikina”,
alisema Mwigulu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), wilaya ya Meatu
Elizabeth Kabati alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakishindwa
kugombea nafasi za uongozi kwa hofu ya familia zao kurogwa.
“Jamii bado inaamini kuwa endapo unataka kugombea nafasi ya uongozi
lazima uende kwa mganga wa kienyeji ili mambo yako yawe sawa. Baadhi ya
wanaume wanapata hofu kuwa wake zao na familia zao zitaandamwa kurogwa
na hivyo kusababisha familia iingie kwenye matatizo matokeo yake familia
zitajihusisha na vitendo vya kishirikina”
,aliongeza Kabati.
“Tunaendelea kuielimisha jamii kuwa Uongozi siyo lazima kushika dawa
bali kinachotakiwa ni Kumwamini Mungu na kuishirikisha familia na jamii
ikukubali,jamii ikukubali lazima itakuunga mkono na utafanikiwa kuwa
kiongozi katika jamii”
,alisema Kabati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa VIKOBA kata ya Mwamishali wilaya ya
Meatu,Enock John alisema ni kweli kuna baadhi ya wanaume wana imani
potofu wanasema haiwezekani mtu kusimama mwenyewe akajiamini na kuwa na
ujasiri bila kushika dawa katika uongozi wa kisiasa.

Aliwataka wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kuwa na nguvu
ya ushawishi katika jamii huku akieleza kuwa ili ufanikiwe unatakiwa
kumjua Mungu kwani mtu mwenye hofu ya Mungu ana maadili mema.

“Wanawake ni jeshi kubwa,mwanamke ni kiongozi tangu kuzaliwa kwake
hata katika familia mwanamke ndiyo nguzo kuu,kutokana na uwezo wake
anatakiwa kuwa kiongozi ili kusaidia kuleta maendeleo yenye tija katika
jamii”
,aliongeza.