Wanawake 102 kupatiwa mafunzo ya udereva

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akifungua mafunzo ya udereva kwa
wanawake 102 yanayofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),
jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo
wanawake kuwa madereva mahiri wa mabasi makubwa hapa nchini.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), Prof. Zacharia  Mganilwa, akitoa taarifa ya utendaji
wa chuo hicho kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi
Isack Kamwelwe (hayupo pichani), kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya udereva
kwa wanawake 102 yanayofanyika  jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti
wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Gillard Ngewe, akizungumza na
wanafunzi  madereva wanawake 102 (hawapo pichani), watakaopatiwa mafunzo
hayo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es
Salaam.
Mwakilishi wa Madereva Wanawake
Bi. Martha Mimbi, akikabidhi risala kwa niaba ya washiriki  kwa Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, mara baada
ya kufungua mafunzo maalumu ya madereva hao, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akiwa katika picha ya pamoja na
madereva wanawake 102  yatakayofanyika katika Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya madereva wanawake 102  watakaopatiwa mafunzo hayo katika Chuo cha
Taifa cha Usafirishaji (NIT), wakifurahi baada ya kufunguliwa kwa
mafunzo hayo rasmi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Mhandisi Isack Kamwelwe, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amefungua mafunzo ya udereva kwa
wanawake 102 yatakayofanyika katika Chuo cha Usafirishaji cha Taifa
(NIT) jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yamelenga
kuwajengea uwezo wanawake kuwa madereva mahiri wa mabasi na hivyo kuwa
chachu katika kuboresha usafiri nchini.
Akifungua mafunzo hayo ya siku
arobaini na tisa yanayofadhiliwa na Benki ya Dunia, na kuratibiwa
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Waziri Kamwelwe,
amesema kuwa mpango huo wa mafunzo umekuja wakati muafaka kwani Serikali
inahitaji wataalamu wenye weledi katika miradi ambayo inaendelea
kutekelezwa hapa nchini. 
“Serikali ya Awamu ya Tano
inaendelea kuijenga Nchi ya Uchumi wa Viwanda ambapo imewekeza nguvu
kubwa katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ikiwemo upanuzi wa
barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha, ujenzi flyover ambayo
imekamilika, ujenzi wa interchange Ubungo, pamoja na Mradi wa
Mabasi yaendayo kwa Kasi (BRT) na hivyo miundombinu hii inahitaji
madereva wenye ueledi katika kuilinda na kuiendeleza”, amefafanua Waziri
Kamwelwe.
Ameongeza kuwa fursa hiyo
imetolewa kwa wanawake kwa kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa
madereva wanawake ni makini zaidi wawapo barabarani. 
“Nimefanya kazi kwa miaka
mingi lakini sijawahi kuona au kusikia mwanamke amefika ofisini akiwa
amelewa hivyo naamini tunaandaa wataalam wenye maadili na kazi yao”,
amesema Waziri Kamwelwe. 
Waziri Kamwelwe amefafanua
kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana katika kuimarisha usalama wa usafiri
kwa njia ya barabara kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi yetu.
Awali akitoa taarifa Mkuu wa
Chuo cha NIT, Mhandisi Prof. Zacharia M.D. Mganilwa,  amemueleza Waziri
huyo kuwa Chuo kimepanga kuendelea na mafunzo hayo pamoja na kuanzisha
mafunzo ya waendesha mizani ili kusaidia kupunguza changamoto za kukosa
watalaamu mahiri wa masuala hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe, amesema ana imani kuwa madereva hao
watakapomaliza  mafunzo hayo watakuwa waaminifu, wadilifu na wazalendo
katika kulinda rasilimali ambazo watanzania kupitia kodi zao wamewekeza
ili kuchangia maendeleo ya Taifa letu. 
Naye, Kamanda wa Polisi wa
Kikosi cha Usalama Barabarani Taifa Fortunatus Muslim, amesema kuwa
mpango huu umekuja wakati muafaka ambapo nchi inaelekea kukua kuelekea
uchumi wa kati na kupanua miundombinu yake. 
Amesema kuwa ni wakati sasa wa
kutoa uelewa kuwa udereva ni taaluma na sio kimbilio la wale waliokosa
ajira  kwani taaluma hiyo inabeba maisha ya watu. 
Ameongeza kuwa ana imani
wanawake waliochaguliwa wataleta mabadiliko makubwa kwani tafiti
zinaonyesha kuwa katika ajali 110 madereva waliopoteza maisha  walikuwa
madereva 109 ni wanaume na dereva mmoja ni mwanamke.