Watanzania waishio na vvu waaswa kuendelea kutumia dawa za kufubaza virusi

Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy
Mwaluko akizungumza na wajumbe wa Baraza la watu wanaoishi na virusi vya
UKIMWI wa KONGO ya Wilaya ya Kilombero alipowatembelea kuangalia namna
wanavyoendesha shughuli zao za kimaendeleo na kuwajulia hali tarehe 17
Oktoba, 2019.
Mwenyekiti
wa Konga ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wilayani ya Kirombero
Halida Ally akimuonesha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko bidhaa mbalimbali wanazotengeneza
katika Konga yao ikiwa ni sehemu ya miradi inayowasaidia kujipatia
kipato na kuinua uchumi wao alipotembelea konga hiyo Oktoba 17, 2019.
Mkurugenzi
wa Utafiti na Tathimini kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania
(TACAIDS) Dkt. Jerome Kamwela akizungumza jambo kuhusu hali ya
Maambukizi mapya kwa wanakonga ya Wilaya ya Kilombero wakati wa ziara ya
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi.
Dorothy Mwaluko.
Mratibu UKIMWI mkoa wa Morogoro Bi. Ndayahunda Hendry akizungumza jambo wakati wa mkutano huo.
Baadhi
ya wanachama wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU wa KONGA ya Kilombero
awakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko (hayupo pichani) wakati wa ziara yake
katika ofisi za konga hiyo, Oktoba 17, 2019.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
……………….
NA.MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uwekezaji, Dorothy Mwaluko amewaasa
Watanzania wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kuendelea
kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo ili waweze kuishi maisha yenye
afya na amani wakati wote.
Ametoa kauli hiyo wakati
akizungumza na wanachama wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya
UKIMWI katika Konga ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mkoani
alipowatembelea kukagua utekelezaji wa majukumu ikiwa ni pamoja na namna
konga hiyo inavyoendesha shughuli za uzalishaji Wilayani hapo Oktoba
17, 2017 Mkoani Morogoro.
“Kipekee ninawapongeza kwa ujasiri
wenu wa kujitokeza na kuonesha ulimwengu kuwa janga hili lipo na ni
letu sote, kwani naamini hakuna mtu ambaye halijamgusa kwa namna moja au
nyingine hivyo niwaombe mjitahidi kuendelea kutumia dawa hizi za
kufubaza makali ya virusi ili kuendelea kuimarika zaidi,”alisema
Mwaluko.
Aliwasisitiza kuendelea kuwa
mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawajatambua hali zao na wale
waliotambua hali zao kuendelea kufubaza virusi na kutoacha kutumia  dawa
hizo kwa kuzingatia umuhimu wake.
“Napenda kuwahamasisha msiache
wala kuchoka kutumia dawa hizi kwa kuzingatia umuhimu wake katika
kuhakikisha zinawapa nafuu na kuondoa magonjwa nyemelezi kuendelea kuwa
na afya njema na kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kufanya
dunia mahali salama pa kuishi,”alisisitiza Mwaluko.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Utafiti na Tathimini kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS)
Dkt. Jerome Kamwela aklieleza kuwa, hali ya kiwango cha maambukizi Mapya
ni asilimia 4.7 Kitaifa na maambukizi hayo ni mengi kwa wanawake kuliko
wanaume hivyo Serikali itaendeelea kuhudumia kundi hili kwa kuhakikisha
lilapewa dawa hizo kwa kadri itakiwavyo.
“Serikali imejipanga kuhakikisha
kundi la WAVIU wote wanahudumiwa na kupatiwa mahitaji yao muhimu ikiwemo
upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi (ARV) hivyo na
kuhakikisha kundi kubwa la wanawake ambao ndiyo wanaoathiriwa zaidi
linafikiwa kadiri iwezekanavyo na hii itaendeelea kusaidia kundi hilo
kupunguza hatari ya kuingia katika maambukizi mapya,”alieleza
Dkt.Kamwela.
Aliongezea kuwa takwimu zinaonesha
hali ya maambukizi mapya kwa kila mwaka ni watu 72000 ambapo kundi la
vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 linaongoza kwa asilimia 40 na
kueleza kundi la wanawake wanachangia asilimia 80 ya maambukizi hayo.
“Serikali imetoa kipaumbele kuwa
mwitikio wa masuala ya UKIMWI umelenga kundi la vijana ili kupunguza
maambukizi mapya yanayolikumba kundi hilo,”alifafanua Dkt.Kamwela.
Aliongezea kuwa wananchi
wasipotambua hali zao mapema wanasababisha kuanza tiba kwa kuchelewa na
hivyo kulazimika kuanza dawa wakati wa hatari na kuwalazimu kuwa na
juhudi za ziada katika kutumia dawa ili kutokomeza maambukizi mapya na
kufubaza virusi vya UKIMWI.
Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Watu
wanaoishi na virusi vya Ukimwi wa Konga hiyo Halida Ally alieleza kuwa
hali ya utoro wa dawa imechangia kuongezeka kwa maambukizi mapya ambapo
walifanikiwa kuhamasisha watu 30,712 kupima hali zao ambapo jumla ya
watu 2,038 walikutwa na maambukizi kati yao wanawake ni 1,327  na
wanaume ni 711.
Alisema hali ya utoro wa dawa ni
changamoto katika kuhudumia kundi hilo inayochangiwa na uwepo wa sababu
mbalimbali ambapo katika kundi la WAVIU 2,038 wanaotumia dawa za
kufubaza virusi ni 1,707 kati yao wanawake ni 1,034 na wanaume ni 673
katika kundi hilo watoro wa dawa ni 996 kati yao wanaume ni 335 na
wanawake ni 673 hali ambayo inachangia kuongezeka kwa maambukizi mapya
na kuongeza ukubwa wa janga hilo katika Halmashauri yao.
Naye mmoja ya wanachama wa konga
hiyo Betina Januari aliipongeza Serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali katika mapambano dhidi ya Ukimwi na kuahidi uendelea kutoa
ushirikiano katika jitihada za kuwawekea mazingira wezeshi na kufikia
malengo ya sufuri tatu ifikapo 2030.
KONGA Kilombero ni Baraza la Taifa
la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) ngazi ya Wilaya. KONGA ya
Kilombero imeundwa mwaka 2013 ikiwa na vikundi 14 vyenye jumla ya
wanachama 354 ambapo wanawake ni 237 na wanaume 117.