Watumishi wa afya waaswa kutoshiriki kwenye uhalifu wa kuharibu ushahidi

Na Englibert Kayombo, WAMJW – Moshi Kilimanjaro.

Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile amewaasa watumishi wa afya kutoshiriki kwenye makosa
ya uhalifu kwa kuharibu ushahidi wa makosa ya jinai pindi wanapofanya
uchunguzi wa kitaalam.


Dkt.
Ndugulile ametoa kauli hiyo alipokuwa ziarani katika Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) akizungumza na watumishi wa afya
hospitalini hapo.

“Katika
kosa ambalo hatutamsamehe mtumishi wa afya ni kushiriki katika uhalifu
wa kuharibu ushahidi, hatutamvumilia mtu ambaye atashiriki kwenye makosa
hayo” alisema Dkt. Ndugulile.

Alisema
kuwa kesi za ukatili wa kijinsia mara nyingi huwa ni kesi za jinai huku
wataalam wa afya wakipewa dhamana ya kuthibitisha ukweli wa matukio
hayo na kuwataka kufuata miiko na maadili ya taaluma ya afya.

“Mtu
amepata shambulio, daktari unasema kwamba huyu mtu hajashambuliwa,
tumeshawahi kufanya hiyo na endapo tukithibitisha pasipo na shaka kwamba
wewe mtaalam wetu umeenda kinyume na miiko na maadili ya kazi yako
lazima tutakuchukulia hatua” alisisitiza Dkt. Ndugulile.