Waziri hasunga: tutafanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya kilimo

Na Mathias Canal, Telaviv-Israel

Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali YA Tanzania
imejipanga kuikabili sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa
kuwaandaa watanzania katika kubadilisha kilimo chao kutoka kwenye
kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara.


Waziri
Hasunga ameyasema hayo  tarehe 3 Septemba 2019 wakati akizungumza na
Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima katika Ofisi za
Ubalozi huo zilizopo katika mtaa wa 12, Abba Hillel Silver Jijini Tel
Aviv nchini Israel.

Alisema
kuwa katika ziara yake hiyo amejifunza namna ambavyo nchi ya Israel
imepiga hatua ya ujuzi katika sekta ya kilimo hivyo kuona umuhimu wa
serikali ya Tanzania kuwekeza katika skimu za umwagiliaji.

Alisema
kuwa asilimia kubwa ya wakulima nchini Tanzania wanatumia majembe ya
mkono katika kilimo jambo ambalo haliwezi kuongeza tija na uzalishaji.
“Tunatumia majembe ya mkono mbaya zaidi kilimo chetu kinategemea msimu
wa mvua, hivyo kilimo cha namna hiyo bado kinatuchelewesha, tuna wajibu
wa kujifunza kwa wenzetu walioendelea” Alisema Mhe Hasunga

Alisema
kwa kuanza serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa kilimo
inaweza kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza
uwezo wa kilimo cha umwagiliaji kitakachofanya kazi msimu mzima badala
ya kilimo cha kutegemea mvua.

Mhe
Hasunga alisema kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kadhalika wizara ya Viwanda na Biashara zitafanya kazi
kwa pamoja ili kuona namna ya kuzalisha kwa tija mazao ya kilimo na
kutoa malighafi nyingi zitakazochangia katika kuinua na kuchagiza
matakwa ya serikali ya kuwa na serikali ya viwanda.

Kuhusu
masoko ya mazao yanayozalishwa nchini Tanzania Mhe Hasunga alisema kuwa
serikali inaendelea na mkakati maalumu wa kuimarisha masoko kwani
imeanzisha kitengo maalumu katika wizara ya kilimo kitakachokuwa na
wajibu wa kushughulikia masoko ya mazao ya wakulima.

Katika
hatua nyingine Waziri Hasunga ameyaalika makampuni mbalimbali ya Israel
yanayojishughulisha na kilimo kutembelea nchini Tanzania kwa ajili ya
kujionea fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.

“Tanzania
ni nchi yenye rutuba nzuri, eneo kubwa kwa ajili ya uwekezaji wa
kilimo, hivyo nayaalika makampuni yote yanayohusika na kilimo hususani
yanayojishughulisha na utafiti, kutembelea Tanzania kwani ni nchi yenye
eneo zuri na kubwa kwa ajili ya uwekezaji hususani katika sekta ya
kiliumo” Alikaririwa Mhe Hasunga

Mhe
Hasunga amesema kuwa Israel ni nchi yenye eneo dogo kwa ajili ya kilimo
lakini wanazalisha chakula kinachotosheleza wananchi wake sambamba na
kuuza mazao yao nje ya nchi jambo ambalo linaimarisha pato la serikali
ya nchi hiyo na kipato cha mtu mmoja mmoja.

Vilevile,
waziri Hasunga ameupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Israel
unaoongozwa na Mhe Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima
na watendaji wengine wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya uwakilishi wa
Tanzania, Aidha Mhe Hasunga amemuomba Balozi huyo kutafuta fursa zaidi
za makampuni ya kilimo na viwanda kwa ajili ya kuwekeza nchini Tanzania.

Kwa
upande wake Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima
amesema kuwa miongoni mwa mambo muhimu ya kuyafanyia kazi ni pamoja na
kutafuta namna ya kuongeza idadi ya vijana wanaoshiriki katika mafunzo
ya kilimo ya Agro Studies ili izidi kuongezeka maradufu.

Kadhalika,
alisema kuwa ofisi yake inaendelea kufanya kazi kubwa kuongeza idadi ya
watalii wanaotembelea nchini Tanzania kwani idadi kubwa ya watalii
inaongeza pato la kigeni la nchi.

Balozi
Masima alisema kuwa nchi ya Israel ina mafanikio makubwa kwenye sekta
ya teknolojia hivyo ni wajibu wa Tanzania kutumia fursa hiyo muhimu
katika elimu ya ujuzi wa teknolojia za kilimo hususani umwagiliaji.

MWISHO