Waziri lugola kutatua kero za wamiliki, waendesha vyombo vya moto kupitia bonanza kubwa la vijana mkoani dodoma kesho

Na Mwandishi Wetu, MOHA

WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika Bonanza kubwa la Vijana litakalofanyika Chang’ombe jijini Dodoma,
kesho jumapili.


Bonanza
hilo, pia litashirikisha wananchi mbalimbali wakiwemo wamiliki na
waendesha vyombo vya moto kutoka Wilaya zote za Mkoa huo.

Akizungumza
na mwandishi wa habari hii, jijini Dodoma leo, Waziri Lugola alisema
amealikwa na viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
kuwa mgeni rasmi ambao ndio waratibu wa Bonanza hilo.

Lugola
alisema amepewa taarifa na uongozi wa UVCCM Mkoa, kuwa wamejipanga
vizuri na pia Bonanza hilo litaambatana na michezo mbalimbali na
burudani kutoka kwa wasanii wa miondoko ya kizazi kipya.

“Kupitia
mkutano huo wa Dodoma, nitalenga kuwahabarisha vijana wote na wananchi
kwa ujumla hapa nchini, kuhusu mafanikio ya Serikali katika kuwasaidia
vijana kupambana na umaskini, na kutatua tatizo la ajira pasipo
kunyanyaswa kwa kujua au kwakutokujua kwa vyombo vya ulinzi na usalama
hususani jeshi la polisi, pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali,”
alisema Lugola.

Alisema
vijana ni nguzo ya taifa, hivyo Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na
inawathamini katika mazingira yao ya kujipatia kipato ikilenga kuwapa
nafasi mbalimbali ili waweze kupata mafanikio zaidi.

“Mwezi
uliopita nilikutana na wamiliki na waendesha bodaboda na bajaj zaidi ya
2000 mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro, nilitoa mwarobaini wa kero zao,
ambazo nyingi zaidi zilihusu Manispaa ya Moshi kutowatendea vema katika
maeneo mbalimbali ya maegesho ya vyombo vyao vya moto, pamoja na kero
nyingine zilizowahusu baadhi ya askari wangu wa kikosi cha usalama
barabarani ambapo vijana hao waliwalalamikia,” alisema Lugola.

Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Billy Chidagwa alisema
Bonanza hilo litaacha historia katika mkoa huo kutokana na maandalizi
yao waliyoyafanya katika kufanikisha vijana mkoani humo wanakutana
pamoja na kero zao kutatuliwa.

Chidagwa
alisema vijana mbalimbali watakuwepo katika tukio hilo, hasa wanaotumia
vyombo vya moto mbalimbali vikiwemo Bajaj, Bodaboda na waendesha
daladala kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.

“Tumejipanga
vizuri kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi mbalimbali wakiwemo
Mbunge wa Vijana, Mbunge wetu wa Jimbo, viongozi wa chama, tunaamnini
uwepo wao kutakuwa na tija kufanikisha tukio hili ambalo maandalizi yake
ni ya muda mrefu, na tayari yamekamilika,” alisema Chidagwa.

Alisema
Bonanza hilo litaambatana na michezo mbalimbali, ambapo kwa upande wa
mpira wa miguu, timu ya bodaboda itacheza na timu ya Askari Polisi
mkoani Dodoma.

“Vijana
njooni kwa wingi kesho jumapili tarehe 22 mwezi huu wa tisa pale
Chang’ombe ili tufurahi kwa pamoja na kumsikiliza mgeni wetu rasmi,
ambaye ni Waziri Lugola atakapotatua kero zetu na kutuonyeshea njia ya
mafanikio zaidi katika Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt.
Magufuli,” alisema Chidagwa.

Waziri
Lugola ambaye alikuwa mkoani Arusha kikazi, amewasili leo jijini Dodoma
kwa ajili ya kufanikisha tukio hilo muhimu kwa maendeleo ya vijana.