Waziri lukuvi awataka wakurugenzi wa halmashauri kujitathmini katika utoaji hati za ardhi

Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA
Waziri wa Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka
wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuanza kujitathmini katika idadi ya
hati za ardhi wanazotoa kwa wamiliki wa ardhi kwenye halmashauri zao.

Alisema Wizara yake itaanza kutangaza wilaya itakayoongoza katika
Upangaji, Umilikishaji na Utoaji Hati za ardhi kwa wananchi ili kubaini
hamashauri ambazo ziko nyuma katika kutoa hati za ardhi kwa wananchi.

Lukuvi alisema hayo jana katika mkutano wake wa kusikiliza na kutatua
kero za ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Iringa kupitia programu ya Funguka
kwa Waziri uliyofanyika ukumbi wa Siasa ni Kilimo katika Manispaa ya
Iringa,

‘’Mkurugenzi ajione fahari kuwaezesha wananchi kwa kupima na kuwapatia
hati, kama Mkurugenzi huwezi kutoa hati miliki hata mia moja basi wewe
hufai’’ alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, kumilikisha na kumpatia mwananchi hati ya ardhi ni
kumuwezesha kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia hati kwenye shughuli za
kimaendeleo na kusisitiza kuwa wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe
wanapanga na kuwamilikisha maeneo wananchi.

Aidha, Lukuvi alisema kwa sasa wizara yake imejipanga kuhakikisha
inasogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za
mikoa zitakazokuwa na watendaji wote wa sekta ya ardhi kama vile
Wapimaji, Wathamini, Wataalamu wa Mipango Miji pamoja na Wasajili.

‘’Sasa Wapimaji, Wathamini na Wapangaji watakuja hapa Iringa, muundo
unaanza mwezi ujao lengo ni kuwapunguzia usumbufu wananchi katika kupata
huduma za ardhi’’ alisema Lukuvi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, katika kuboresha
huduma za sekta ya ardhi, Wizara yake itatumia mifumo unganishi
itakayorahisisha utendaji kazi kwa wataalamu wa sekta ya ardhi ambapo
kazi kubwa itakuwa ikifanyika kielektroniki badala ya kutumia makaratasi
aliyoaeleza kuwa wakati mwingine husababisha tamaa kwa maafisa ardhi.

Alitolea mfano mkoa wa Dar es Salaama kuwa, ushaanza kutumia mfumo
unganishi ambapo sasa wamiliki wa ardhi katika mkoa huo wanapatiwa hati
za kielectroniki na kubainisha kuwa lengo la kuwa na mfumo unganishi ni
kuondoa urasimu na kurahisisha utendaji kazi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi alieleza kuwa mkoa wake
umejitahidi kupunguza kero na migogoro ya ardhi iliyokuwepo miaka ya
nyuma kwa kuanzisha utaratibu wa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao
kupitia programu ya Iringa Mpya.

Alimueleza Waziri Lukuvi kuwa, kama angekuja mwaka mmoja na nusu
uliopita basi ukumbi aliofanyia mkutano wa Funguka kwa Waziri ungekuwa
umejaa wananchi wenye kero za ardhi lakini jitihada za mkoa wake
zimesababisha mkutano huo kutokuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye
migogoro ya ardhi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

‘’Muda mwingi nautumia kwenda kwa wananchi na kazi za ardhi zina
changamoto kubwa na njia pekee ya kukabiliana nazo ni kutenda haki bila
kujali uwezo, kabila ama dini ya mtu’’ alisema Hapi.