Waziri mkuu aagiza miundombinu ya shule ikamilike mapema….asema kama kuna wahusika walioko likizo warudishwe haraka

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya
shule ikamilike mapema na kama kuna watendaji walioko likizo warudi
kwani Serikali inataka wanafunzi wote waanze masomo pamoja.


Ameyasema
hayo jana (Jumanne, Desemba 31, 2019) wakati alipofanya ziara kukagua
ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleoa wilayani Ruangwa. Amesisitiza
ukamilishwaji wa miradi hiyo ili wananchi waanze kuitumia.

Waziri
Mkuu amesema agizo alilolitoa kwa wakuu wa mikoa Desemba 29, 2019
kuhusu usimamizi wa miundimbinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa liko
pale pale kwa sababu Serikali haitaki kuona wanafunzi wakipishana
katika kuanza masomo.

Miradi
ambayo Waziri Mkuu ameitembelea ni ujenzi wa shule ya msingi ya Ng’au
ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, ujenzi wa chuo cha VETA,
hospitali ya wilaya ya Ruangwa na shule ya sekondari ya Lucas Maria.

Waziri
Mkuu amesema Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo hivyo ni lazima viongozi katika maeneo husika wahakikishe
wanashirikiana katika kusimamia utekelezaji wake.

Amesema
wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020,
hivyo ni lazima usimamizi ukaongezwa katika baadhi ya maeneo ambayo
miundombinu yake bado haijakamilika ili kuwahi masomo.

Akiwa
katika shule ya Sekondari ya Lucas Maria Waziri Mkuu amemuagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Andrea Chezue
ahakikishe mafundi wanafanya kazi usiku na mchana.

“Shule
zinakaribia kufunguliwa na baadhi ya majengo kama bwalo, maabara,
nyumba za walimu hayajakamilika mafundi hawapo eneo la ujenzi na
Serikali imetoa fedha. Nataka kazi hii ikamilike mapema kwani hakuna
sababu.”

Wakati
huo huo, Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa wamepongeza na kumshukuru Rais
wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na miradi ya
kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wananchi
hao wakiwemo vijana wanaojenga chuo cha VETA walitoa pongezi na
shukrani hizo mbele ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza kukagua mradi wa
ujenzi wa chuo hicho. Mafunzo yatakayotolewa chuoni hapo ni pamoja na
ufundi uashi, seremala, magari, ushonaji nguo na Tehama.

Kadhalika,
vijana hao wamewashauri vijana wenzao wajitokeze na kuchangamkia fursa
za ajira zinazopatikana katika maeneo yao kupitia miradi mbalimbali
inayotokelezwa na Serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi.