Waziri mkuu afuta mnada wa nafaka ulioendeshwa na tra

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefuta mnada wa nafaka ulioendeshwa na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA)  Januari 7, 2020 na kuuagiza uongozi wa mamlaka
hiyo kutangaza upya zabuni baada ya kutoridhishwa na taratibu
zilifanyika awali.


Mnada
huo ambao unahusisha mahindi tani 5,000 na ngano tani 460.12 unafanyika
baada ya wahusika kushindwa kutimiza masharti ya kiforodha, hivyo
Serikali imeamua kuuza ili kufidia gharama zake. Nafaka hizo ziliingia
nchini Machi 2017.

Waziri
Mkuu amesitisha mnada huo jana (Alhamisi, Januari  9, 2020) wakati
akizungumza na Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA, Bw. Ben
Asubisye, ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es Salaam.

Waziri
Mkuu ameagiza kutangazwa upya kwa mnada mwingine wa kuuza mahindi hayo
sambamba na ngano na wahakikishe masuala yote kuhusu mnada huo
yanakamilika ndani ya siku tatu kuanzia  tarehe 09 Januari 2020.

“Mahindi
yameuzwa kwa bei ya sh. 340 kwa kilo moja ambayo ni chini na bei ya
soko kwa sababu bei ya mahindi sokoni kwa sasa ni sh. 800. Zabuni
imetangazwa kwa muda mfupi watu wameshindwa kushiriki. Ilifunguliwa saa 8
mchana na imefungwa saa 5 usiku.”

Kadhalika,
Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa TRA uhakikishe mnada unaofuata unakuwa
wa wazi, huru pamoja na kutoa muda wa kutosha kwa wananchi wote
kushiriki ili kuondoa malalamiko.

“Kwa
kuwa mnada unafanyika kwa njia ya mtandao, hakikisheni matumizi ya
mtandao yanakuwa rafiki kwa wananchi wote watakaovutiwa kuwasilisha
zabuni zao.”

Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa TRA ishirikiane na mamlaka nyingine
za Serikali kuhakikisha wanunuzi wa nafaka hizo hawaziingizi sokoni kwa
ajili ya matumizi ya binadamu. Nafaka hizo zimepimwa na kuthibitika
kuwa zinafaa kwa matumizi ya wanyama.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU