Waziri mkuu: wakulima msiuze pamba chini ya sh. 1,200


WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa zao la pamba nchini
wasikubali kuuza pamba yao chini ya bei elekezi ya sh. 1,200.


Hata
hivyo, Waziri Mkuu amewashauri wafanyabiashara wa zao hilo waungane na
kuanzisha viwanda vya kutengeneza nyuzi na nguo ili kuongeza thamani
kabla ya kuuza pamoja na kuwahakikishia wakulima soko.

Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 21, 2019) wakati
akizungumza na viongozi na wananchama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha
Chato  (CCU) pamoja na wananchi kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha
Chato kinachomilikiwa na CCU mkoani Geita.

Amesema
wakulima waendelee kuwa na subira kwa sababu wanunuzi hao wamepewa
fedha za kutosha kununua pamba yote kwa bei ya 1,200 na si vinginevyo.

“Hata
mkiwa na shida msikubali kuuza pamba yenu chini ya sh. 1,200 kwa kuwa
haitachukua muda mrefu mtakuwa mmeshapata fedha zenu. Tuna taarifa kuwa
kuna wanunuzi wamepata fedha na wanawatumia watu kwenda kuwalaghai
wakulima kwa kutaka kununua kwa bei ya sh. 800, msikubali na mkiwaona
mtupe taarifa.”

Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema viwanda vya nyuzi na vya nguo vikijengwa nchini
vitakuwa na uhakika wa soko kwani hivi sasa Tanzania  haina viwanda vya
kutosha vya nguo. Amesema Serikali ipo tayari kuwaunga mkono Watanzania
wote au mwekezaji yeyote atakayekuwa tayari kuanzisha viwanda vya aina
hiyo kwa sababu mahitaji ni makubwa.

“Tuna
shule zaidi ya 18,000 Tanzania na wanafunzi wote wanavaa sare
zinatokanazo na pamba, tukisema majora ya sare yasukwe humu humu ndani
na kisha kusambazwa mikoa yote bado nguo za watu wanaovaa mitaani.
Watapata faida tu.”

Pia,
Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wote wa vyama vya ushirika katika
maeneo yanayolima pamba kuwaelimisha wakulima kuhusu umuhimu wa
kuzalisha pamba safi ili walinde heshima ya pamba ya Tanzania ambayo
duniani inasifika kuwa ni dhahabu nyeupe.

Awali,
Meneja wa CCU, Charles Nyasi alimwambia Waziri Mkuu kuwa makampuni ya
METEL, KCCL na FRESHO yamejitokeza kununua pamba kupitia AMCOS na tayari
kilo 9,611,860 zimenunuliwa  kati ya kilo 11, 140,529 zilizokusanywa.

Alisema kampuni ya FRESHO imenunua kilo 4, 869, 960, KCCL imenunua kilo 3, 025,051 na METEL imenunua kilo 1,716, 420.

Pia
Meneja huyo aliiomba Serikali  isaidie kuwalipia deni la sh.
696,854,475.20 ili kumaliza tatizo la madai ya watumishi na wadai
wengine. Pia aliiomba Serikali isaidie kuilipia CCU deni la sh. 102,
942,300.00 la ardhi waliyotumia kujengwa kiwanda chao.

Akijibu
maombi hayo Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli haiwezi kulipa deni hilo hadi itakapopewa
maelezo ya kina ni nani aliyesabaisha deni, mazingira yaliyosababisha
deni hilo.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,