Waziri wa kilimo abaini ubadhilifu bodi ya korosho, aunda tume kuchunguza

WAZIRI
wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi kwenye mfuko wa wakfu wa
kuendeleza zao la Korosho baada ya kubaini kuwepo na udanganyifu.


Mhe
Hasunga amemuagiza CAG kuchunguza kiasi cha Shilingi Bilioni 53.2
kilichobaki kwenye akaunti ya Mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao la
Korosho ambazo zilikuwa kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu vya kubangua
korosho na maghala.

Aidha
Mhe Waziri ameunda timu ya watu wasiozidi watano kwa ajili ya kuhakiki
kiasi cha korosho kilichopokelewa na kilichouzwa katika msimu wa Korosho
wa mwaka 2018/2019 baada ya kubaini uwepo wa udanganyifu.

Hayo
ameyasema jana tarehe 17 Novemba 2019 jijini Dodoma mbele ya wandishi
wa habari ambapo amezitaka pia kamati za ulinzi na usalama kusimamia
zoezi la uhakiki ambalo linaonekana kutawaliwa na udanganyifu ambapo
timu iliyoundwa itashirikiana na timu iliyokuwepo chini ya wizara hiyo
kuhakiki pia fedha zilizopatikana ili wahakikishe wanaolipwa ni wale
wanaostahili.

Aidha
amesema timu hiyo ihakikishe kuwa majina yaliyotoka kwenye vyama vya
msingi kwenda kwenye vyama vikuu hadi fedha zilizoingia benki  kama
kweli ziliingia kwenye akaunti za wakulima na kama kuna unyaufu
uliojitokeza wabainishe ni kwa kiwango gani ili kusaidia serikali kutoa
taarifa yenye uhalisia.

Waziri
Hasunga amesema mwaka 2016 serikali iliamua kufuta mfuko wa Wakfu na
kwenye akaunti kulikuwa na kiasi cha shilingi bilioni 53.2 lakini bodi
ya Korosho iliamua kubadili matumizi na kutumia fedha hizo tofauti na
maagizo yaliyotolewa na serikali.

“Kama
Wizara hatupo tayari kuona ubadhilifu wowote wa fedha za umma
unafanyika, Serikali ya awamu ya tano haiwezi kukubali kuona watu
wachache wanafaidika na fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Timu
zote mbili naziagiza hadi kufikia Januari 15 mwaka 2020 wawe
wameshatuletea ripoti wizarani. Niwahakikishie hatutomvumilie yeyote
ambaye atajaribu kugusa fedha za wananchi, ” Amesema Waziri Hasunga.

Amesema
bodi hiyo ilitumia kiasi cha shilingi bilioni 28.1 kununua
viuatilifu,walitumia kiasi cha shilingi bilioni 12.2 kulipia magunia
ilhali katika msimu huo wanunuzi walikuwa wananunua magunia wao wenyewe.

Ametoa
wito kwa wakulima kuwa kama kuna anayedai ushirika apelike madai yao
kwenye kamati ya ulinzi na usalama na timu iliyoundwa ili waseme kama
hawajalipwa.