Hasira na wasiwasi
unaongezeka miongoni mwa wakaazi wa mataifa mengi barani Ulaya kutokana na
kurejea tena kwa vizuizi vikali vya kukabiliana na maambukizi pamoja na vifo
vya COVID-19.
Katika kile kinachoonekana kuwa ishara za kukata tamaa,
waandamanaji kwenye miji kadhaa nchini Uhispania mwishoni mwa wiki walipambana
na vikosi vya usalama kupinga kurejeshwa kwa marufuku ya shughuli za kawaida
kujaribu kupambana na kitisho cha virusi vya corona.
Hivi
sasa Uhispania inatekeleza amri ya kutotoka nje usiku na karibu majimbo yote ya
nchi hiyo yameifunga mipaka ya ndani kuzuia safari za masafa marefu.
Serikali
barani Ulaya zinahangaika kupunguza ongezeko la kutisha la maambukizi ya virusi
vya corona ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 279,000 barani humo tangu
vilipozuka nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.
Nchini
Uingereza, wengi wameelezea wasiwasi walio nao kuhusu hasara ya kiuchumi
itakayopatikana katika muda wa wiki nne ambao shughuli zote za kawaida
zitafungwa.
Huko
Italia ambako kulishuhudiwa maandamano makubwa wiki iliyopita, serikali
inatarajiwa kutangaza hatua mpya za vizuizi baadae hivi leo.
Duru
zimearifu serikali inalenga kupiga marufuku safari baina ya majimbo nchini
humo, kufunga maduka makubwa, kupunguza shughuli za biashara na kuzuia watu kutoka
nje usiku.
Ujerumani nayo kuweka vizuizi vipya
Ujerumani hayo imeanza leo kutekeleza awamu mpya ya vizuizi
ikiwa ni pamoja na marufuku ya mikusanyiko, kufungwa kwa kumbi za starehe na
maduka yasiyo na bidhaa zinazohitajika kwa wingi pamoja na msisitizo kwa watu
kuvaa barakoa.
Meneja
wa mkahawa mmoja nchini Ujerumani aliyejitambulisha kama Christian Lehner
amesema:
“Athari
za kiuchumi wala hazipimiki tena. Mwaka huu wote unapaswa kusahaulika. Inafaa
kuusahau mwaka huu mzima. Kabla ya marufuku ya kwanza, mwezi Februari, hakukuwa
na cha kuingiza kwa sababu kila kitu kilishindana. Hata msimu wa kiangazi,
ambako kwa baadhi ya wakati bustani zilijaa watu, ilikuwa ni sawa na tone
kwenye bahari. Sasa tunaingiza sehemu tu ya kile tunachohitaji kuishi. Mwaka huu
siyo wa kutengeneza tenapesa. Ni mwaka wa kujiokoa tu kiuchumi, kulinda ajira
na kampuni.”
Kwengineko
waziri mkuu wa Ufaransa Jean Castex amesema kuanzia kesho Jumanne maduka
makubwa yatapigwa mafuruku kuuza bidhaa ´zisizo muhimu´ kama ilivyokuwa kwa wauzaji
wadogo waliolazimika kufunga maduka yao.
Mkuu wa WHO yuko Karantini
Wakati huo huo, mkuu wa shirika la Afya duniani, WHO, Tedros
Adhanom Ghebreyesus, amesema anajiweka karantini baada ya kukutana na mtu
ambaye sasa amebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Akiandika
kupitia ukurasa wake wa Twitter, Tedros amesema bado yuko na afya njema bila
dalili za COVID-19 lakini atasalia karantini kwa siku kadhaa zinazokuja kama
taratibu za WHO zinavyoelekeza.
Tedros
amesema ni muhimu kuzingatia miongozo ya wataalamu wa afya kwa lengo la
kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona na kuikinga mifumo ya afya kutozidiwa
na idadi ya wagonjwa.
Wiki
iliyopita mkurugenzi huyo wa WHO aliwatolea wito viongozi wa dunia kuzingatia
ushauri wa wataalamu katika wakati idadi ya maambukizi inapanda barani Ulaya na
kwenye mataifa ya Amerika Kaskazini.