Na Stela Paul
Wananchi wa kijiji cha Kiloleli Kata ya Kiloleli katika halmashauri ya Wilaya
ya Kishapu Mkoani Shinyanga wamefanikiwa kuanzisha ujenzi wa choo chenye
matundu 24 na chumba kimoja cha kujisitili wanafunzi wa kike katika Shule ya
Msingi Kiloleli.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana wananchi
wa kijiji hicho wamesema wamefanikiwa kuazisha ujenzi huo baada ya kituo cha taarifa na maarifa kuibua changamoto
zinazoikabili shule hiyo na kuwahamasisha katika zoezi la uchangiaji.
Mmoja kati ya wananchi wa kijiji hicho Martha
Ngwelu amesema wameanzisha ujenzi huo kutokana na upungufu wa matundu ya choo unaosababisha
wanafunzi kujisaidia katika mazingira yasiyo rafiki.
“Wanakituo cha taarifa na maarifa walitupa
hamasa baada ya kuibua changamoto hii na kuchangia mifuko mitano ya saruji
pamoja na shilingi 50,000 ndipo na sisi wananchi tukaanza zoezi la kuchangia
maana tulikuwa tunasema tu kwenye mikutano ya hadhara lakini kuchangia hamna,
kwahiyo tunaomba serikali itushike mkono ili kukamlisha ujenzi huu” amesema
Ngwelu
Kwa upande wake Mwanakituo cha taarifa na
Maarifa namba 9 kata ya Kiloleli Helena Makelele amesema wameibua changamoto ya
upungufu wa matundu ya choo katika Shule hiyo na kuwashirikisha wananchi
kupitia Bunge la jamii na wananchi wakahamasika katika uchangiaji.
“Tulikuwa
na Bunge la jamiii tukawashirikisha wananchi jinsi watoto wetu wanavyohangaika,
wanajamii waliitikia nguvu ya wananchi ikaanza kuchimba mashimo, sisi kama
wanakituo cha taarifa na maarifa tulitoa shilingi 50, 000 na mifuko mitano ya
saruji. Wananchi walituunga mkono wakaanza kuchangishana, walianza na mchango
wa shilingi 1,000 na badae wakatoa mchango wa shilingi 2,000 mpaka tumefikia
hatua hii” amesema Helena.
Joseph Solea ni mwana kituo cha taarifa na maarifa katika kijiji cha Kiloleli ameeleza namna walivyoibua changamoto ya
upungufu wa matundu ya choo katika shule ya msingi Kiloleli na kuchukua hatua ya
kuwashirikisha wananchi ili kuchukua jitihada mbalimbali kwaajili ya ujenzi wa choo
kipya.
“Tuliangalia changamoto zinazozikumba taasisi
mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, tukabaini changamoto kubwa ni upungufu wa
matundu ya choo katika shule hii kwa sababu watoto wanahangaika wakati mwingine
wanakwenda kujisaidia huko chini, tuliwashirikisha wanajamii kupitia vikao
mbalimbali kisha tukaanza ujenzi huu”amesema Joseph.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule
ya Msingi Kiloleli Mwalimu Juliana Petro amesema shule hiyo inajumla ya
wanafunzi 997 ambapo changamoto ya upungufu wa matundu ya choo inachangia
msongamano wa wanafunzi chooni hivyo kuchangia wanafunzi kupitwa na vipindi vya
masomo darasani.
“wanafunzi wanapokwenda chooni wanakuwa wengi
kwa sababu ya kusubiriana kwahiyo inachukua muda mrefu na wanachelewa kurudi
darasani, kukamilika kwa ujenzi huu kutaleta unafuu na kupunguza mlundikano wa
wanafunzi chooni japo matundu bado hayatoshi” amesema Mwalimu Juliana.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Kuhwema Mashara
amesema kuanza kwa ujenzi huo imetokana na michango ilitokusanywa kutoka sehemu
mbnalimbali ikiwemo kituo cha taarifa na maarifa, wananchi, serikali ya kijiji
na Kamati ya maendeleo ya kata WARDC.
“walianza kituo cha taarifa na maarifa
wakachangia, wananchi wakakubaliana tukachangia shilingi 2,000 tukanunua nondo
na saruji na kujenga bampa ,WARDC ikanipa mifuko 30 ya saruji, kwenye serikali
yetu ya kijiji nikatoa shilingi 600,000” amesema Mashara.
Mtendaji wa Kijiji hicho Nicholaus Mzirai amesema
mpaka kufikia sasa wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Milioni 2,500,000 ambapo
ujenzi umefikia kwenye hatua ya lenta.
“Kupitia vikao mbalimbali tulivyozungumza hapo
awali na mpaka sasa jumla ya michango tuliyofanikiwa kukusanya ni shilingi
milioni 2,500,000 na ujenzi umefikia kwenye hatua ya kupigwa lenta” amesema
Mzirai.
Kuanza kwa ujenzi huo ni baada ya wanakituo cha taarifa na maarifa waliojengewa uwezo wa ulagabishi na Mtandao wa
Jinsia Tanzania TGNP kuibua changamoto katika taasisi mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi Kiloleli na kuhamasisha
wananchi kuanza kuchangia shughuli za maendeleo.
Muonekano wa choo cha zamani.Muonekano wa matundu ya choo ambayo yanajengwa na kituo cha Tarifa na Maarifa kutoka Kata ya Kiloleli wilayani Kishapu.