Miraji athumani achaguliwa mchezaji bora ligi kuu ya vodacom mwezi septemba 2019


MSHAMBULIAJI wa timu
ya Simba ya Dar es Salaam, Miraji Athumani amechaguliwa kuwa Mchezaji
Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu
wa 2019/20, huku Patrick Aussems pia wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa
mwezi huo.

 
Miraji na Aussems
walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali
katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya
VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana
na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali, ambavyo
ligi hiyo inachezwa msimu huu. 

 
Kwa mwezi huo wa
Septemba, Simba ilicheza michezo mitatu na kushinda yote ikiifunga
Mtibwa Sugar mabao 2-1, Kagera Sugar mabao 3-0 na Biashara United mabao
2-0, ambapo Miraji alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo
akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio hayo ya Simba ikiwa ni pamoja na
kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mabao mawili. 

 
Miraji aliwashinda
Meddie Kagere wa Simba aliyetoa mchango mkubwa pia katika mafanikio ya
Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne. Mchezaji mwingine
aliyeingia fainali alikuwa Ismail Kada wa Prisons aliyeonesha kiwango
kizuri na kutoa mchango katika michezo ambayo Prisons  ilicheza
ikishinda miwili, sare mmoja, ambapo iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1,
Mtibwa Sugar mabao 3-1 na kutoka sare na Lipuli mabao 2-2.

Kwa kutwaa tuzo hiyo,
Miraji atazawadiwa kikombe na Tsh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka
Vodacom. Vilevile atapata Kisimbusi  kutoka Azam TV.

 
Kwa upande wa Aussems
aliwashinda Mohammed Rishard wa Prisons na Abdallah Mohammed Baresi wa
JKT Tanzania, ambapo Aussems aliongoza timu yake kupata ushindi katika
michezo mitatu, kati ya hiyo mmoja nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar na
miwili ugenini mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar na mabao 2-0 dhidi ya
Biashara United. Simba imemaliza mwezi ikiwa nafasi ya kwanza. 
 

Rishard aliingia
hatua ya fainali baada ya kuiongoza Prisons kushinda michezo miwili na
kutoa sare mmoja, ambapo ilishinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Ruvu
Shooting, kisha ikashinda ugenini mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa na ikatoka
sare ugenini na Lipuli ya mabao 2-2, wakati Baresi aliingoza JKT
Tanzania kushinda michezo miwili, sare moja na kupoteza mmoja.
 

 JKT Tanzania
ilifungwa ugenini bao 1-0 na Lipuli,  ikatoka 0-0 nyumbani na Mtibwa
Sugar,  ikashinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Biashara United na pia
ikapata ushindi ugenini kama huo dhidi ya Kagera Sugar.