Molinga ainusuru yanga kufungwa na polisi tanzania ligi ya vodacom

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
 

YANGA SC imenusurika kupoteza mchezo wa pili mfululizo katika
Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimisha sare ya 3-3 na Polisi
Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
 

Mshambuliaji mpya, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), David Molinga ‘Falcao’ ndiye aliyeinusuru Yanga na fedheha leo
baada ya kufunga mabao mawili kipindi cha pili timu ikitoka nyuma kwa
3-1 na kupata sare ya 3-3.  
 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Mwinyimkuu,
alyesaidiwa na Makame Mdogo na Joseph Pombe, Yanga walitangulia kupata
bao kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji mkongwe, Mrisho Khalfan Ngassa.
 
Mshambuliaji Ditram Nchimbi anayecheza kwa mkopo kutoka Azam
FC akafunga mabao matatu mfululizo kuanzia dakika ya 29, 55 na 58 kuipa
uongozi timu ya kocha Suleiman Matola katika mchezo wa ugenini.


Hata hivyo, Molinga aliye katika msimu wake wa kwanza akafunga
kwa kchwa dakika ya 22 akimalizia krosi kutoka kulia na klwa shuti la
mpira wa adhabu dakika ya 65 kuitoa nyuma Yanga na kufanya mechi iwe
3-3.


Polisi Tanzania wakamalizia dakika tano za majeruhi wakiwa
pungufu ya mchezaji ya mmoja kufuatia Yassin Mustafa kutolewa kwa kadi
nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 90.


Leo Yanga ilicheza bila kocha wake, Mkongo Mwinyi Zahera ambaye
anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu kufuatia tuhuma za kutoa
maneno yasiyofaa baada ya mechi ya kwanza wakifungwa 1-0 na Ruvu
Shooting Agosti 28 hapo hapo Uwanja wa Uhuru. 


Timu iliongozwa na Kocha Msaidizi, Mzambia Noel Mwandila aliyekuwa akisaidiwa na kocha wa makipa, Manyika Peter. 


Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Juma Abdul, Ally
Mtoni ‘Sonso’, Kelvin Yondan, Lamine Moro, Abdulaziz Makame, Mrisho
Ngassa, Feisal Salum ‘Fei Toto’, David Molinga, Juma Balinya/Mapinduzi
Balama dk46 na Sadney Urikhob/Deus Kaseke dk46.


Polisi Tanzania; Kulwa Manzi, William Lucian ‘Gallas’, Yassin
Mustafa, Pato Ngonyani, Iddi Mobby, Baraka Majogoro, Andrew Chamumu,
Hassan Maulid, Ditram Nchimbi, Marcel Kaheza na Sixtus Sabilo/Mohamed
Mkopi dk70.