Mtanzania anayesoma Dubai aanzisha mashindano ya Wanafunzi Sekondari Arusha

  • Lengo kuu ni kuibua vipaji vya wanafunzi
  • Agawa vifaa vya michezo, Timu nane kushiriki

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mtanzania Ashok Mittal (17),  anayesoma elimu ya juu Dubai katika falme za nchi za Kiarabu (UAE),  ameanzisha mashindano ya mpira wa miguu kwa vijana wa shule za Sekondari kwa lengo la kuhamasisha michezo kwa vijana shuleni.

Mashindano hayo yaliyoanza Leo Agosti1,2024 yanayojulikana kama ” Champion of Tomorrow” yameshirikisha timu nane za Sekondari ikiwemo washiriki kutoka Sekondari za Serikali na binafsi.

Shule zinazoshiriki michuano hiyo ni pamoja na Sekondari za Serikali za Lemara, Sombetini, Sinoni na Mateves huku Sekondari binafsi zikiwa ni St.Patrick, Renea, Kilimanjaro modern Boys Academy na Brainy Heroes zote za Jijini Arusha.

Ashok amesema timu zote zinazoshiriki michuano hiyo  zimepata udhamini kupitia kampuni mbalimbali hapa nchini ambapo zitapewa  jozi za viatu vya kuchezea mpira, t-shirt, mpira na gloves kwaajili ya makipa.

“Nina furaha kubwa kuanzisha ‘Champions of Tomorrow Football League’ hapa Arusha. Lengo langu ni kutoa fursa kwa vijana wasio na uwezo kutimiza shauku yao ya mpira wa miguu na hatimaye kufikia viwango vya kitaaluma, kwa kutoa vifaa muhimu vya michezo,” anasema na kuongeza:

“Kwa  kushirikiana na makocha wa timu zote pamoja na baadhi ya wakufunzi kutoka katika vituo vinavyolelea Watoto wenye vipaji vya mpira wa miguu(scout) Jijini Arusha,  tutaweza  kuwawezesha malengo na ndoto za vijana wetu kutimia na kuchangia maendeleo chanya katika jamii yetu,”.

Amesema mpango huo ni juhudi za pamoja kati yake binafsi pamoja na ushirikiano wa misaada kutoka kwa  wadhamini mbalimbali waliojitokeza kudhamini michuano hiyo.

Timu ya sekondari ya Lemara ikifanya mazoezi

Mashindano hayo yanayoendeshwa kwa njia ya mtoano yatafikia kilele chake Agosti 8,2024 ambapo itachezwa fainali kwa timu ambazo zitakuwa zimefanikiwa kufikia hatua hiyo baada ya kupenya katika hatua ya mtoano.

Katika mchezo wa kwanza Leo hii timu za Sekondari ya St. Patrick na Sombetini zilitoshana nguvu kwa goli 2-2 katika mchuano mkali uliofanyika kwenye viwanja vya mpira vya shule ya kimataifa ya UWC.

Ramadhani Abbasi na Emmanuel Masanja ndio walioipatia timu ya Sekondari ya St.Patrick magoli huku Sekondari ya Sombetini ikipata magoli yake kupitia kwa wachezaji wake mahiri Boniface Exaveri na Yusuf Kassim.

katika mchezo wa pili timu ya Sekondari ya Lemara iliinuka kidedea dhidi ya Sekondari ya Kilimanjaro modern Academy kwa jumla ya goli 1-0. Goli hilo la Sombetini Sekondari  lilifungwa na Hajiru Nassoro aliyewazidi ujanja walinzi wa timu ya Kilimanjaro.

Kocha wa timu ya mpira ya Sekondari ya St.Patrik Dennis Shemtoe amempongeza muandaaji wa michuano hiyo na kushauri  kufanyike kwa maandalizi mazuri zaidi hapo baadae kufuatia kuwepo kwa changamoto ya waamuzi wasaidizi.

Wachezaji wa timu za mpira wa miguu sekondari ya Lemara na Kilimanjaro Boys Academy wakipata mawaidha kabla ya mpira kuanza
Mchezo kati ya Sekondari ya Lemara na Kilimanjaro ulipokuwa ukiendelea katika viwanja vya shule ya kimataifa ya mchepuo wa kiingereza ya ISM UWC, Kisongo Jijini Arusha