Yanga kichwa cha ‘mwendawazimu’, yashikwa pabaya na zesco ya zambia, yalazimishwa sare ya 1 – 1

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

YANGA SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zesco United
ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa
kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo
Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.




Matokeo yake yanamaanisha kwamba Yanga inatakiwa kwenda kufanya
ilichokifanya kwenye Raundi ya kwanza kushinda ugenini baada ya sare
kama hiyo nyumbani na Towsnhip Rollers ya Botswana mwezi uliopita. Yanga
ilishinda 1-0 mjini Gaborone.

Katika mchezo wa leo, Yanga SC walitangulia kwa bao la mkwaju wa
penalti la kiungo wake mshambuliaji, Patrick Sibomana dakika ya 24
akimchambua vizuri kipa wa kimataifa wa Zambia, Jacob Banda.




Refa Helder Martin Rodriguez aliyesaidiwa na washika
vibendera Jeeson Emiliano dos Santos na Ivanildo Meirellesde O Sanche
Lopes pamoja na Antonio Caluassi Dungula mezani alitoa penalti hiyo
baada ya Marcel Kalonda kumchezea rafu Mnamibia wa Yanga, Sadney
Urikhob.

Yanga walielekea kabisa kuondoka na ushindi katika mchezo wa leo
kama makosa ya walinzi na kipa wao, Metacha Mnata kumruhusu kiungo wa
zamani wa klabu hiyo, Mzimbabwe Thabani Kamusoko kuisawazishai Zesco kwa
shuti la mbali dakika ya 90 na ushei.




Ni bao ambalo liliwavunja nguvu Yanga na kujikuta wanacheza wakiomba mchezo umalizika kwa sare ya nyumbani. 

Yanga watajilaumu wenyewe kwa sare hiyo, kwani walitengeneza nafasi nzuri za kufunga, lakini wakashindwa kuzitumia.




Timu hizo zitarudiana Septemba 27, mwaka huu mjini Ndola na
mshindi wa jumla ataingia hatua ya makundi, wakati atakayefungwa
ataangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la
Shirikisho. 

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Mapinduzi
Balama/Ali Ali dk74, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro, Kelvin Yondan,
Feisal Salum, Mohammed Issa ‘Banka’/Mrisho Ngassa dk58, Abdulaziz
Makame, Papy Kabamba Tshishimbi, Sadney Urikhob/Maybin Kalengo dk58 na
Patrick Sibomana. 




Zesco United; Jacob Banda, Marcel Kalonda, Simon Silwimba,
Anthony Akumu, John Ching’andu/Kondwani Mtonga dk64, Kasumba Umaru/
Quadri alaedekoun dk73, Thabani Kamusoko, Enock Subumukama/Winston
Kalengo dk37, Jesse Were, Mwila Phiri na Clement Mulashi.