Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Dkt Abdulmajid Nsekela akimshika mkono Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kama ishara ya kumkabidhi pikipiki20 kwaajili ya kuimarisha usalama Mkoani Arusha |
Seif Mangwangi
Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amewataka wahalifu ndani ya Jiji la Arusha kuacha mara moja kwa kuwa Jiji hilo limejipanga kutumia mbinu mbalimbali kupambana nao.
Amesema hivi Sasa Jiji hilo liko kwenye zoezi la kufunga taa na kamera za siri katika mitaa mbalimbali ya Jiji hilo ili kuhakikisha watu wanakuwa salama wakati wote na kuwafanya wananachi wa Arusha kutolala na badala yake wafanye kazi usiku na mchana.
Makonda ameyasema hayo Leo Mei 16, 2024 Jijini hapa wakati akipokea msaada wa pikipiki 20 zilizotolewa na benki ya CRDB kwa lengo la kusaidia kupambana na uhalifu Jijini humo na kuweka mazingira salama ya utalii na wageni mbalimbali wanaotembelea Jiji hilo.
Rc Makonda amesema kwa namna walivyojipanga wahalifu watakuwa wanakamatwa kimya kimya na hivyo kuwataka kutafuta kazi nyingine ya kufanya ili kuepuka mkono wa Sheria.
” Arusha tumejipanga, tuna mpango wa kuongeza pikipiki zingine Hadi kufikia 50, baiskeli 100 zitakazotumia umeme wa jua na magari20, lengo tu ni kupambana na uhalifu, tunataka ukiwa Arusha uhisi kweli Uko sehemu tofauti,” amesema.
Mkuu wa Mkoa Paul Makonda akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya pikipiki20 |
“Nawaomba wateja wa CRDB na wa benki zingine waje wawekeze Arusha kwa kuwa tunahitaji kuwa na migahawa na hoteli za kisasa, na Arusha hivi Sasa ni salama, tumejidhatiti sana na uzuri wale wote ambao walikuwa wakifanya uhalifu tumeshakutana na tumekubaliana watafute kazi ya kufanya, ” amesema Paul Makonda.
Amesema hivi Sasa Arusha inafunguka kibiashara kutokana na kuwa na ongezeko kubwa la wageni na wafanyabishara
Makonda amesema kwa kuwa ameomba usafiri wa pikipiki kwaajili ya Jeshi la Polisi kupambana na uhalifu atahakikisha anafuatilia matumizi ya pikipiki hizo kuzuia uhalifu.
Aidha amesema Jiji la Arusha ni Jiji la utalii hivyo Mkoa umepanga kutumia askari wa JKT kuzuia watu wanaochafua mazingira ili kulifanya Jiji hilo kuwa safi wakati wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Dkt Abdulmajid Nsekela amesema pikipiki hizo zina thamani ya TZS Milioni50 na kwamba msaada huo ni sehemu ya asilimia 1 ya faida inayopatikana katika benki hiyo na kurejeshewa kwa jamii.