Jumuiya a.mashariki kuendeleza ushirikiano na waandishi

Mkurugenzi wa huduma za kijamii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt Iren Isaka akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani kwa Mkoa wa Arusha yaliyofanyika Mei11,2024

Egidia  Vedasto

Arusha

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeahidi kuendelea kushirikiana na waandishi wa habari  kama takwa la kikatiba la Jumuiya hiyo.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari kwa Mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki, jijini hapa, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii katika Jumuiya hiyo Dkt.Irene Isaka ameahidi kuendeleza ushirikiano na Waandishi wa habari Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla ili kuendelea kutangaza mambo mazuri ndani ya Jumuiya hiyo.

Aidha ameeleza kuwa, uhuru wa vyombo vya habari ni kuwajibika na kuandika habari zenye ukweli na uhakika kwa kufuata misingi na miiko ya Uandishi wa habari, pia kuheshimu haki na uhuru wa watu wengine.

“Nawasihi ndugu waandishi wa habari kutumia lugha za staha katika kazi yenu ya kufikisha habari kwa jamii, mkumbuke nchi wanachama wa jumuiya hii wanajifunza kwenu, na Arusha ni kielelezo cha Jumuiya, kwa hiyo waandishi wa mkoa huu ni wa muhimu sana na mnafuatiliwa kwa ukaribu na Jumuiya yetu” amesema Dkt. Irene.

Amesema  kama kauli mbiu ya maadhimisho hayo inavyosema ‘waandishi wa habari na changamoto za tabianchi’, ni kweli nchi za Jumuiya hiyo zimekumbwa na changamoto nyingi za mabadiliko ya tabianchi hivyo waandishi wa habari wanapaswa kuendelea kutoa elimu kuhusiana na utunzaji wa Mazingira ili kuepukana na madhara zaidi kutokanana uharibifu wa Mazingira unaoendelea kufanywa.

K

Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Mobhare Matinyi akizungumzia Maadili katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani Mkoa wa Arusha.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya HabariMaelezo Mobhare Matinyi amewataka waandishi wa habari kurudi shule na kuongeza elimu ili waweze kufanya kazi yao kwa weledi.

Hata hivyo Matinyi amesema kwa miaka mitatu , vyombo vya habari nchini vimeonekana kufanya vizuri Barani Afrika katika  utendaji wake wa kazi, kwa kufuata misingi na maadili ya uandishi wa habari.

Aidha amepongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kusaidia tasnia ya habari nchini.

“Kipekee nawashukuru na kuwapongeza sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ushirikiano wenu wa karibu na vyombo vya habari, naukumbuka mchango wenu mkubwa miezi michache iliyopita mlipoahidi Baraza la vyombo vya habari kuwa muangalizi wa jumuiya hiyo, ni heshima kubwa na ninatambua mchango huo” amefafanua Matinyi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa habari Mkoa wa Arusha Claud Gwandu akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani kwa Mkoa wa Arusha 

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na wadau wa habari katika kuhakikisha tasnia ya habari inafaidisha pande zote ikiwemo mzalishaji wa habari na mlaji kwa kuzingatia maadili.

Kwa upande wake mmoja wa waliotoa mada katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa chama cha Waandishi Mkoani Mwanza (MPC) Edwin Soko, amesema waandishi wanatakiwa kufuata kanuni, taratibu na miiko ya uandishi wa habari ili kuepuka migogoro na migongano katika jamii 

“Nawakumbusha  mkumbuke kuzingatia sheria za uandishi hususan kipindi hiki tunapoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani” ameeleza Soko na kuongeza:

“Nawakumbusha kujua haki zenu na mipaka katika utendaji kazi, kuzingatia sheria za uchaguzi, kutokuwa na upendeleo, kuwasilisha maoni ya demokrasia bila upendeleo, kuepuka uchochezi, kuepuka kukashifu, kuheshimu maoni ya wawasilishaji kwa njia mubashara na kwa ujumla mnatakiwa kuishi na sheria zote” amesisitiza Soko.

Meneja wa TCRA Kanda ya Kaskazini Dkt Francis Mihayo akizungumza na Waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha wakati wa maadhimisho ya Siku siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani kwa Mkoa wa Arusha yaliyofanyika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Wakati huo huo Meneja Mawasiliano Kanda ya Kaskazini Dkt. Francis Mihayo amesema mamlaka hiyo inasimamia sheria na kanuni za mawasiliano ya huduma za simu, intaneti, utangazaji na Posta.

Sambamba na hayo Dr. Mihayo amewataka waandishi wa habari kuendelea kufuata na kuzingatia kanuni za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tunatekeleza majukumu yetu kwa kufuata Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotutaka kuhakikisha jamii inaunganishwa na mawasiliano, haijalishi mjini au vijijini, amesoma au hajasoma, ni haki ya msingi huduma hiyo kupatikana na waandishi wa habari ni miongoni mwa waunganisha mawasiliano kupitia habari” amesema Mihayo.

Wadau mbalimbali pamoja na Waandishi wa Habari walioalikwa wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa