Waziri kairuki,kitila wakutanisha wadau wa utalii arusha

 

Egidia Vedasto

Arusha

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema, Afrika bado ina mchango mdogo katika ukuaji wa utalii duniani hivyo jitihada kubwa zinahitajika.

Akifungua Kongamano la uwekezaji kwenye Sekta ya Utalii katika Mkoa wa Arusha lililofanyika Jijini Arusha,  Mkumbo amesema Bara la Afrika Lina mchango mdogo  katika suala zima la ukuaji wa utalii ukilinganisha tofauti na mchango mkubwa wa utalii kutoka Bara la Ulaya.

Aidha, Prof Mkumbo amesema ifikapo Julai 1 mwaka huu atakuwa Arusha kwa ajili ya kufungua kituo Cha uwekezaji, kwa lengo la kuimarisha zaidi sekta ya  uwekezaji na kukuza utalii kwa ujumla.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo katika Mkutano wa Wadau wa Utalii Jijini Arusha

Prof Mkumbo ametaka kuundwa kwa timu ya kuchukua maoni, changamoto na zile zinazofaa kutatuliwa na watendaji wa Utalii na zile ambazo zinapaswa kutatuliwa na ngazi ya Uwekezaji  ili zitatuliwe mapema iwezekanavyo.

“Katika bara la Afrika tuna mchango mdogo sana katika ukuaji wa Utalii ni kama asilimia ndogo  hivyo sekta ya utalii bado tunapaswa kufanya bidii sana ili kukuza utalii duniani” amesema Mkumbo.

Wakati huo huo, Waziri  wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki amesema bado kuna Kazi kubwa kuhakikisha wanafikia malengo ya  ongezeko la watalii kufikia milioni tano Kwa Mwaka wa fedha 2024/2025, na kwamba huku akisema kuwa umebaki mwaka mmoja ambao ni muda mchache, hivyo kunahitajika Kasi ya juu  kufanikisha jambo hilo.

“Bado matamanio yetu ni  kufikia malengo ya kupata  watalii milioni tano kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na muda wa mwaka mmoja uliobaki ni mchache na ukizingatia mpaka sasa watalii walioingia nchini ni  milioni 1.8  hivyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya”amesema Kairuki.

Amesema  wako katika harakati ya kuboresha maeneo ya uwekezaji katika utalii hasa katika Miundombinu ya malazi na hoteli pamoja na kituo cha kisasa cha mikutano kinachojengwa na Kituo cha mikutano cha kimataifa  cha AICC kinachotarajia kubeba watu 10000 kwa wakati mmoja.

Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi  Iman Nkuwi, amesema lengo la Kongamano hilo ni kuwakutanisha wawekezaji kwenye Sekta ya Utalii kujadiliana Kwa pamoja namna gani  wanakwenda kuboresha  na kuimarisha  sekta ya Utalii hususani  katika suala Zima la uwekezaji wa miundombinu Mbalimbali Katika mkoa wa Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amesema ana mpango wa kuibadilisha mandhari ya arusha na kuwa ya kiutalii kwa kufanya mabango yote kuwa ya kielekitroniki.

“Nataka Arusha iwe ya dola na sio shilingi, hata muuza mchicha na muendesha bodaboda ajivunie mkoa huu wa utalii, ili hata wageni kutoka nje wakiingia wafurahie mandhari ya Arusha” amesema Makonda.

Kongamano la Uwekezaji wa Utalii Nchini limefanyika jijini Arusha na kuwakutanisha Wadau mbalimbali wa Utalii.

_Wadau mbalimbali katika mkutano wa Sekta ya Uwekezaji na Utalii leo Jijini Arusha