Na Mapuli Misalaba,Shinyanga
Watoto wawili wakazi wa kata ya Ndala wanafunzi wa sekondari wanashikiliwa na jeshi la Polisi kwa mahojiano kufuatia tuhuma ya kuhusika na wizi wa vipande 12 vya mabati.
Watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Ndala anasoma shule ya sekondari Ndala mwingine mwenye umri wa miaka 15 mwanafunzi wa shule ya sekondari Mwasele kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga, ambao wamekamatwa kufuatia doria ya jeshi la jadi sungusungu la mtaa wa Mwasele B, wakiiba mabati kwenye nyumba iliyokuwa ikipauliwa.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mwasele B Cosmas Lukas amesema hatua ya kukamatwa vijana hao ni mpango mkakati unaolenga kudhibiti tabia za uhalifu katika mtaa huo ikiwemo vitendo vya wizi, udokozi na vibaka.
“Changamoto kubwa niliyonayo ni vibaka na sasa tunapambana nao kwa nguvu zote tumeanza kuwakamata hawa tumewaleta kituo cha polisi na tunaendelea hatutaacha mpaka tuhakikishe tunalitokomeza kabisa suala ya wezi kwenye mtaa wangu”.
Mwenyekiti huyo amesema serikali ya mtaa wake itahakikisha inadhibiti mianya yote ya uharifu kwa kuwa wanaojihusisha na vitendo hivyo ni vijana wanaoishi katika maeneo hayo.
“Hawa wezi tunahakikisha tunapambana nao hawataweza hili nalisimamia na hii mara nyingi tunasumbuliwa na wanafunzi wanatoka nyumbani kwao wakiwa wamevaa nguo za shule wakifika mtaani wanabadillisha sasa tumeanza na hawa wawili tutaendelea kuwakamata mpaka uhalifu utakapoisha “.
Akizungumza Babu wa mmona wa kijana ambaye yuko mahabusu kwa tuhuma za wizi ameeleza masikitiko yake akisema kuwa hakujua kama mjukuu wake anajihusisha na tabia za wizi kwa kuwa ni mwanafunzi amekuwa akiaga nyumbani kwamba anaelekea shuleni kumbe alikuwa akijihusisha na vitendo vya uhalifu.
“Zimenishtua sana taarifa za mjukuu wangu asubuhi anavaa yunifomu nampa na hela ya chakula shuleni matokeo yake shuleni hafiki anaishia kwenye masuala ya wizi akifika darajani anavua nguo za shule anaingia mtaani kuiba mimi namshukuru sana mwenyekiti kwa kumkamata akishirikiana na Jeshi la Polisi vitu ambavyo nilikuwa sivijui sasa nimevijua kumbe huyu mjukuu wangu anatatizo la wizi”.
Mzee huyo ametoa ushauri kwa wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kufuatilia mienendo yao wawapo nyumbani na shuleni ili kuwadhibiti wasijihusishe na vitendo vya uhalifu.