Serikali kufanyia kazi mbagala kuwa mkoa wa kikodi

Na. Saidina Msangi na Josephine Majura, WFM, DodomaSerikali
imesema kuwa inafanyia kazi ombi la Mbunge Mbagala la kuifanya Mbagala
kuwa Mkoa wa kikodi ili kurahisisha ulipaji wa kodi ikiwemo ya Majengo.


Hayo yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la
nyongeza la Mbunge huyo , Mhe. Issa Ali Mangungu, aliyetaka kujua ni
lini Serikali itaifanya Mbagala kuwa Mkoa wa Kikodi ili kuwalahisishia
wananchi kulipa kodi.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, suala la Mbagala kuwa Mkoa wa Kikodi
linafanyiwa kazi ili kuhakikisha shughuli za ukusanyaji wa kodi
zinafanywa kwa ufanisi na kwa urahisi.

Alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA ilikusanya takribani Sh.
Bilioni 3.7 katika mkoa wa kikodi wa Temeke katika mwaka wa fedha
2017/2018, ikiwa ni matokeo ya  marekebisho ya sheria ya fedha ya
Mamlaka ya Serikali za Mitaa kufanyika kupitia sheria ya fedha ya mwaka
2016.

“Mkoa wa kikodi temeke umekusanya kodi kwa asilimia 60 ya lengo la kukusanya takribani Sh. Bilioni 6.1,”alieleza Dkt. Kijaji.

Kwa upande mwingine Dkt. Kijaji, amezitaka Benki zote nchini kuwahudumia
walemavu wanapofika kupata huduma za fedha na pia kurekebisha
miundombinu ya kuingia ATM ili kukidhi mahitaji ya walemavu.

Akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti maalum Mhe. Amina Saleh
Mollel, kuhusu mpango wa Serikali katika kuhakikisha ATM zinakidhi
mahitaji ya walemavu, Dkt. Kijaji alisema kuwa inaangalia namna ambayo
itawezesha   mifumo ya miamala kwa njia ya ATM inakuwa Rafiki kwa
makundi yote wakiwemo watu wenye ulemavu.

“Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha ATM za
mabenki zinawekewa mifumo inayokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu”,
alisema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Mei 2017 Benki Kuu ya Tanzania ilitoa mwongozo
wa mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao ikiwa ni mpango wa Serikali wa
kuhakikisha kuwa huduma za malipo kwa njia ya mtandao zinafanyika kwa
usalama na kukidhi mahitaji ya makundi yote katika jamii.

Aidha pamoja na Serikali kutoa mwongozo huo Benki nchini hazijafanikiwa
kusimika ATM maalum na rafiki kwa watu wenye ulemavu hususan watu wenye
ulemavu wa macho hivyo Benki zinatakiwa kutatua changamoto hiyo.